HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 21 January 2019

KLABU ZA FEMA ZACHANGIA UFAULU WA WANAFUNZI MASHULENI

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
KATIKA kusherekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa  shirika lisilo la kiserikali la FEMINA, mchango wa shirika hilo umeonekana kwa vijana hasa kwa kuonesha juhudi zao za kuwafikia vijana nchini kote na kuwapa elimu kuhusiana na afya ya uzazi, uwezeshaji kiuchumi pamoja na ushiriki katika masuala ya uraia.

Akizungumza na waandishi wa habari katika warsha uliowakutanisha, Mkurugenzi wa Habari wa FEMINA Amabilis Batamula amesema kuwa miaka 20 ya shirika hilo imekuwa ya mafanikio makubwa kwani tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999 vijana wengi wamenufaika na wanaendelea kulea vijana wapya na kusema kuwa programu zote zitakuwa endelevu.

Akieleza maeneo ambayo wao kama FEMINA wanayafanyia kazi Amabilisi amesema kuwa wanajiegemeza katika maeneo makuu matatu ambayo ni kutoa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia ambayo ilianza kutolewa mwaka 1999 kwa kutoa elimu kuhusia na ugonjwa wa UKIMWI na baadae stadi za maisha na taarifa kuhusu afya ya uzazi na kwa sasa katika shule wanatumia mbinu ya kusubiri pamoja na kufikia huduma za afya.

Pia eneo jingine ambalo wanaliegemea ni uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana ambapo huwapa taarifa za fursa zinazowazunguka  vijana hao na sio pesa wala mitaji na hiyo ni katika kuwasaidia kwa kuwajengea wigo wa kujitegemea na katika hilo hushirikiana na wadau mbalimbali wa kimaendeleo katika kupata taarifa ambazo wao huzichakata.

Ameeleza kuwa FEMINA pia hutoa elimu kwa vijana kuhusu kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii kama mikutano ya kata, vijiji na Wilaya pamoja na kujitolea katika nafasi mbalimbali kama vile kufanya usafi katika hospitali, masoko na kujitolea damu na hiyo ni pamoja na kupiga vita tamaduni potovu ikiwa ni pamoja na ukeketaji na ndoa za utotoni.

Amabilisi amesema kuwa lazima wazazi pamoja na walezi wawe wawazi kwa vijana ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha kuhusiana na afya ya uzazi pamoja na kukabiliana na changamoto katika ukuaji wao.

Kuhusiana na mchango wa FEMINA katika klabu za FEMA kote nchini Afisa ufuatiliaji na tathimini kutoka FEMINA Martha Samwel amesema kuwa ufaulu kwa shule zenye klabu za FEMA uameongezeka na hiyo ni kutokana na mirejesho wanayoipata kutoka kwa walimu na walezi wa klabu hizo kwani kupitia klabu hizo wanafunzi wamekuwa wakielimishana na kuhimizana kuhusu masomo na katika baadhi ya maeneo wanafunzi watoro darasani wamerudi shule kutokana na nguvu ya klabu za FEMA.

"Kuna baadhi ya shule zimekuwa na misimamo yao ambapo wanakauli mbiu zao za kutoruhusu mwanaklabu ya FEMA afeli darasani, hii inawapa nguvu na ari ya wao kusoma zaidi na hatimaye kufanya vizuri katika masomo yao" ameeleza Martha.

Aidha amesema kuwa mafanikio waliyoyapata kwa miaka 20 ni makubwa sana hasa kwa kuwafikia vijana wengi Tanzania kote na kutoe elimu ambayo imewasaidia kwa kiasi kikubwa hivyo wanajivunia kuwa sehemu ya maisha kwa  vijana hao.

Pia amewashauri vijana wengine kujiunga na klabu za FEMA ili waweze kupata elimu ya afya na ujinsia pamoja na elimu ya ujasiriamali ambayo itawasaidia katika kujenga taifa na kujenga nchi ya viwanda kwa kuwa wao ndio nguvu kazi ya taifa.
 

Mkurugenzi wa habari wa FEMINA, Amabilis Batamula akizungumza na wanahabari katika warsha iliyowakutanisha  na kujadili  changamoto na mafanikio ya shirika hilo wakielekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.
Mmoja wa waandishi wa habari akiwasilisha mada katika warsha hiyo iliyofanyika katika ofisi za FEMINA jijini Dar es salaam.
Waandishi wa habari wakijadiliana katika makundi kuhusiana na namna vyombo vya habari vinavyochangia kuleta maendeleo nchini.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad