HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 8, 2019

IFAHAMU TAASISI YA WAJIBU NA NAMNA INAVYOHAMASISHA UWAJIBIKAJI NA UTAWALA BORA

 Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
KATIKA kujenga taifa lenye mlengo wa uwajibikaji pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma kwa manufaa kwa wote taasisi ya WAJIBU imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu pamoja na kukuza uwajibikaji na utawala bora nchini.

Mtazamo na dhima ya taasisi ya WAJIBU vinaenda sambamba na na kasi na mlengo wa serikali wa awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kuhusu uwajibikaji na utawala bora pamoja na kupiga vita masuala ya rushwa na ufisadi.

WAJIBU ni taasisi ya ya fikra ya uwajibikaji wa umma iliyoanzishwa mwaka 2015 ikiwa na malengo mbalimbali hasa kukuza uwajibikaji na utawala bora hapa nchini na kushikilia dira ya usimamizi faafu na bora zaidi wa rasilimali za umma kwa manufaa ya wote.

Taasisi ya WAJIBU imebeba dhima ya kuendelea kukua kama taasisi ya fikra ya uwajibikaji ambayo inaongeza thamani katika huduma inazotoa ili kuweza kufanikisha ustawi wa uwajibikaji na utawala bora nchini katika sekta mbalimbali za umma.

Katika kutekeleza majukumu yao taasisi ya WAJIBU inasimamia misingi ya kiutendaji na hiyo ikiwa ni pamoja na kujali watu na kuwahudumia watanzania ambao ndio walengwa wa mambo yote yanayohusu uwajibikaji na utawala bora nchini na wanaamini haki katika kuwahudumia wananchi ni moja ya msingi katika kutekeleza uwajibikaji na utawala bora.

Aidha WAJIBU ni taasisi ambayo haifungamani na upande wowote kisiasa, kijamii na kidini bali wao hutekeleza yale yanayohusu uwajibikaji pamoja na kuangalia masuala ya usawa, uvumilivu na uwazi sambamba na kuwajibika.

Kwa miaka michache tangu kuanzishwa kwake taasisi ya WAJIBU imefanyia kazi ripoti mbalimbali za uwajibikaji ambazo zimewavutia wengi na kuwafungua macho wananchi wengi ambao walikuwa wanasikia ripoti pekee ila uchambuzi kutoka WAJIBU umetoa elimu kwa wengi zaidi,kazi zilizofanywa na taasisi ya WAJIBU ni pamoja na; kuandaa na kusambaza ripoti za uwajibikaji zilizo katika lugha rahisi yenye kueleweka kwa wananchi wa kawaida na ripoti hizo hutolewa kila mwaka nchini.

Aidha taasisi ya WAJIBU huandaa machapisho ya uwajibikaji kwa sekta mbalimbali kama vile sekta ya elimu, maji na afya ambayo husaidia sana katika kuangalia utendaji kwa sekta moja moja.
Kubwa zaidi taasisi ya WAJIBU hutoa mafunzo ya uwajibikaji kwa madiwani, bodi za wakurugenzi wa mashirika ya umma na wabunge pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa halmashauri pamoja na taasisi za kiserikali kuhusiana na masuala ya uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma.

Pia taasisi ya WAJIBU huandaa makongamano ya uwajibikaji katika vyuo mbalimbali ambapo hutoa elimu wa kwa wanafunzi wa vyuo kuhusu kupiga vita masuala ya rushwa na ufisadi na hiyo yote ni katika kuwaandaa ili waweze kuwa viongozi bora na wawajibikaji hapo baadaye.

Vilevile taasisi ya WAJIBU imekuwa ikishirikiana na serikali, Bunge pamoja na AZAKI zinazofanya kazi katika kuhimiza uwajibikaji hapa nchini na wamekuwa wakiandaa makongamano ya uwajibikaji kitaifa yanayojadili hali ya uwajibikaji hapa nchini pamoja na kuandika vitabu mbalimbali vya uwajibikaji na utawala bora.

Katika kuendelea kuhakikisha taifa linajengwa na wawajibikaji na watawala bora WAJIBU wamejipanga kufanya kazi nyingi zaidi hapo mbeleni na kwa kiasi kikubwa zitaleta mabadiliko makubwa katika jamii na hiyo itakua ni pamoja na kuandaa ripoti za hali za uwajibikaji kitaifa ambayo itasaidia kujua namna sekta mbalimbali zinavyofanya kazi kwa kuzingatia utawala bora na uwajibikaji.

Pia WAJIBU imejipanga katika kufanya makongamano mbalimbali kupitia wiki ya AZAKI na kujadili kuhusu uwajibikaji katika kuinua uchumi wa nchi kupitia sera ya nchi katika kujenga Tanzania ya viwanda. Pia WAJIBU wataendelea kuandaa mafunzo kwa AZAKI na madiwani pamoja na kuongeza ushirikiano zaidi na vyombo vya habari katika kuhakikisha taarifa zinawafikia wananchi nchini kote.

Kitu kikubwa ambacho kitaleta mapinduzi zaidi kutoka WAJIBU ni kufanya kazi zaidi na TAMISEMI, TAKUKURU, Ofisi ya CAG, PPRA, TEITI pamoja na Bunge na vyombo vya habari katika kutoa elimu ya uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa hapa na hii italeta matunda kwa wananchi na nchi katika kula keki ya taifa kwa usawa.

Kwa ujumla taasisi ya WAJIBU ni mkono imara ambao utaisaidia serikali ya sasa katika kufikia malengo yake, uwajibikaji na utawala bora ndio nguzo zitakazopeleka taifa mbele zaidi, kwa malengo yao na nia ya serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda ni dhahiri kuwa mafanikio yapo karibu kuyafikia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad