HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 24, 2018

WADAU WA ELIMU WACHANGIA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 250 UJENZI WA MADARASA BUSEGA SIMIYU

Na Stella  Kalinga, Simiyu
Wadau mbalimbali wa elimu wamechangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu katika Harambee iliyofanyika Mjini Nyashimo, ambapo zimepatikana jumla ya shilingi 254, 969,000/= fedha taslimu zikiwa ni shilingi 15,360,000/= ahadi shilingi 241,809,000/= na mifuko ya saruji 127.

Akiongea na wadau hao Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo ambaye alialikwa kama Mgeni rasmi wa Harambee hiyo, Luteni Kanali Josephat Mshashi, Mkuu wa Kikosi cha 27 Makoko Musoma amesema upo umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata elimu kwa kuwa elimu ni urithi hivyo kila mmoja awe na uchungu wa kuona watoto wanasoma.

“Hakuna urithi tunaoweza kuwapa watoto wetu zaidi ya elimu tusipowapa elimu rasilimali zote ambazo tunazipigania leo hii, tunavyopambana kulikomboa Taifa letu kiuchumi itakuwa kazi bure kwa sababu tutabaki na Taifa la watu ambao ni watumwa wa watu wenye elimu” alisema Mshashi

Awali akitoa taarifa ya hali ya vyumba vya madarasa  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njinginya amesema halmashauri hiyo ina upungufu wa vyumba vya madarasa 107.

Mmoja wa Wadau wa elimu katika Wilaya ya Busega, Bw. Deo Kumalija ambaye alichangia katika harambee hiyo ametoa wito wadau wa maendeleo na wananchi kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo waliyopo, ikiwemo ujenzi wa shule kwa kuwa maendeleo yao yataletwa na wao wenyewe.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ameupongeza uongozi wa wilaya ya Busega kuandaa harambee hiyo huku akiwataka kusimamia fedha zilizopatikana, ili zifanye kazi iliyokusudiwa, na kuwasisitiza wazazi, walezi na jamii yote kwa ujumla kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kwenda kidato cha kwanza wanaenda shule.

“Nawapongeza sana viongozi wa wilaya ya Busega wakiongozwa na Mhe. DC kwa kuandaa harambee hii, fedha hizi mhakikishe zinasimamiwa vizuri na zifanye kazi iliyokusudiwa, lakini pia mhakikishe watoto wote waliochaguliwa wanaenda shule, haiwezekani juhudi kubwa namna hii ifanyike kuchangia halafu watoto wasiende shule” alisema Mtaka.

Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka kuwa Viongozi watasimamia fedha yote iliyopatikana na kuhakikisha inafanya kazi itakayokuwa na thamani halisi ya fedha hiyo(value for money).

Akitoa shukrani kwa viongozi na wadau mbalimbali wa elimu waliochangia katika harambee hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Busega, Mhe. Vumi Magoti ametoa wito kwa madiwani kuwahamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kata zao, ili fedha zilizopatikana ziweze kuwasaidia katika ukamilishaji.

Pamoja na kutafuta wadua wa elimu waliochangia zaidi ya shilingi milioni 70 katika harambee hiyo Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe. Dkt. Raphael Chegeni amesema kwa kushirikiana na wadau ameshatoa vifaa vya ujenzi ikiwemo mabati 1700 na mifuko ya saruji 640 ambavyo vimeshasambazwa na kusaidia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani humo.
 Wadau wa elimu na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Simiyu wakichangia katika harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Busega, iliyofanyika Mjini Nyashimo lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa wilayani humo.
 Mkuu wa Wilayaya Busega Mhe. Tano Mwera (kushoto) na Mbunge wa Busega,Mhe. Dkt. Raphael Chegeni wakiteta jambo katika harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Busega, iliyofanyika Mjini Nyashimo lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa wilayani humo.
 Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo ambaye alialikwa kama Mgeni rasmi wa Harambee hiyo, Luteni Kanali Josephat Mshashi, Mkuu wa Kikosi cha 27 Makoko Musoma akizungumza na wadau wa elimu, katika harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Busega, iliyofanyika Mjini Nyashimo lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa wilayani humo.
 Wadau wa elimu na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Simiyu wakichangia katika harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Busega, iliyofanyika Mjini Nyashimo lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa wilayani humo.
 Mdau wa Maendeleo katika Wilaya ya Busega, Bw. Deo Kumalija akichangia katika harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Busega, iliyofanyika Mjini Nyashimo lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa wilayani humo.
Kutoka kushoto Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, mhe. Dkt. Seif Shekalaghe na Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe. Dkt. Raphael Chegeni  wakiteta jambo, katika harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Busega, iliyofanyika Mjini Nyashimo lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa wilayani humo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad