HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 6, 2018

Tanzania kuwakilishwa na waogeleaji wanne Mashindano ya Dunia China

Tanzania itawakilishwa na waogeleaji wanne katika mashindano ya dunia ya kuogelea yaliyopangwa kufanyika nchini China kuanzia Desemba 11 mpaka 16 eneo la Hangzhou Olympic and International Expo Center. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Kuogelea nchini (TSA), Asmah Hilal aliwataja waogeleaji hao kuwa ni Kalya Temba na Celina Itatiro kwa upande wa wanawake na Collins Saliboko na Hilal Hilal watawakilisha upande wa wanaume.

Asmah alisema kuwa kocha maarufu nchini, Alexander Mwaipasi na Mwenyekiti wa chama chao, Imani Dominick wataambatana na timu hiyo nchini China. Alisema kuwa Kayla na Celina wameondoka jana usiku wakati Collins ataungana na wenzake mjini Hangzhou akitokea Uingereza na Hilal atakenda China akitokea Dubai.

Alisema kuwa waogeleaji hao wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo ambayo pia yataambatana na mkutano mkuu wa Shirikisho la Mchezo wa kuogelea duniani (Fina) na kozi ya makocha, Mkutano Mkuu wa Fina na kozi ya makocha utaanzia kesho.  “ Ni matarajio yetu kuwa watafanya vizuri pamoja na changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, mashindano yatakuwa magumu kwani waogeleaji nyota wa Dunia nao watakuwepo,” alisema Asmah.

Mashindano hayo ya 14 yatafanyika kwenye bwawa la kuogelea la mita 25 ambalo ni la kisasa zaidi limejengwa na kampuni ya Italia ya Myrtha Pools na linahamishika. Bwawa hilo la kuogelea limejengwa kwenye uwanja wa tenisi na litaondolewa na kuwekwa eneo la wazi ambalo litatumiwa na jamii.
Waogeleaji wa Tanzania, Celina Itatiro (wanne kutoka kushoto) na Kayla Temba (wa tatu kutoka kulia) katika picha ya pamoja na uongozi Chama cha kuogelea na nchini (TSA) na wazazi mara baada ya kuondoka jana kwenda Hangzhou, China kushiriki mashindano ya Dunia. Katikati ni kocha wa timu hiyo, Alexander Mwaipasi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad