HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 4 December 2018

SERIKALI YAOMBWA KUWEKA JICHO LA PEKEE KUNUSURU ZAO LA NGOZI

Umoja wa Wataalam Wasaidizi Tanzania (TAVEPA), umeiomba Serikali kuweka mkakati wa makusudi wa kunusuru zao la ngozi kwa kuwa sasa hivi hakuna soko la uhakika la zao hilo.
Mwenyekiti wa (TAVEPA) Bw. Salim Msellem, alisema hayo leo (03.12.2018) Jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 14 wa wataalam wasaidizi wa afya ya mifugo nchini.

“Ngozi nyingi hutupwa, kitu ambacho kinaletea hasara taifa kwa kukosa fedha za kigeni, pia kudhoofisha uchumi wa mfanyabiashara mmoja mmoja wa ngozi hapa nchini,” alisema Bw. Msellem. Alisema pia lazima kuwe na mkakati wa dhati wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata ngozi utasaidia kunusuru zao la ngozi.

Akizungumzia uwezo mdogo wa wahitimu wa stashahada ya afya na uzalishaji mifugo (DAHP), alisema, TAVEPA imepata malalamiko toka maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu suala hilo. “Wahitimu wa DAHP imebainika muda wa mwaka mmoja wa masomo ya stashahada ya afya ya Mifugo (DAHP) hautoshi, ombi letu tunaomba stashahada iwe kama awali, ya miaka miwili au miaka mitatu na msisitizo uwe mafunzo kwa vitendo ili kumuandaa mhitimu kufanya kazi kwa ufanisi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Kwa sasa inaonekana wanasoma kwa ajili ya kwenda vyuo vikuu na siyo kwenda kuwasaidia wafugaji kule vijijini, hakika uwezo wao kwa vitendo ni mdogo sana,” alisema Bw. Msellem. Aidha umoja huo umeiomba serikali kuandaa mkakati wa dhati wa kusimamia mafunzo rejea kwenye tiba, matumizi sahihi ya dawa, ukaguzi wa vyama, ubora wa ngozi na ubora wa wanyama wanaotaka kuchinjwa kwa watumishi wa umma na sekta binafsi mara kwa mara ili kuwajengea uwezo.

Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Mifugo (TVA), Prof. Dominic Kambarage, alisema Tanzania ina ng'ombe wengi na inauza ng'ombe hizo nchi mbalimbali za Afrika Mashariki hivyo ni vyema wafugaji wakachangamkia Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Prof. Kambarage alisema ni vyema sasa wafugaji wakapewa elimu ya kutosha pamoja na upatikanaji wa chanjo za mifugo ili kudhibiti magonjwa pamoja na kupata masoko ya uhakika ili kila mtu anufaike na rasilimali hiyo.  "Sekta ya mifugo ni sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi na Tanzania ni ya pili Barani Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, hivyo mifugo hiyo ikitumika vyema itasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuongeza kipato, " alisema.

Naye Msajili wa Baraza la  Veterinari (VCT) nchini, Dkt. Bedan Masuruli, alisema ni vyema kudhibiti magonjwa yatokanayo na mifugo kwani asilimia 70 ya magonjwa ya kupe yanaua mifugo hivyo ni vyema wafugaji wakaogesha mara kwa mara mifugo yao ili kudhibiti ugonjwa wa kupe.
 Prof. Dominic Kambarage akitoa maelezo juu ya umuhimu wa sekta ya mifugo nchini kwa wanachama wa Umoja wa Wataalam Wasaidizi Tanzania (TAVEPA) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 14 wa wataalam wasaidizi wa afya ya mifugo nchini uliofanyika Jijini Arusha.
Wanachama wa TAVEPA wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi   (Hayuko pichani).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad