HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 24 December 2018

SERIKALI YAJIPANGA KUHAKIKISHA HUDUMA YA MAJI INAFIKA KOTE NCHINI IFIKAPO 2021

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii

WAZIRI wa maji na umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa ametoa muhtasari wa mwaka kuhusiana na suala la maji na kuwahakikishia kila mtanzania anafikiwa na huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Waziri wa  Profesa. Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali imejipanga katika kuhakikisha ifikapo mwaka 2021 wananchi kwa asilimia 95 wanapata maji safi na salama na hiyo ni katika kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi na kueleza kuwa tenda ya kutekeleza miradi ya maji kwa Miji na Wilaya itatangazwa mapema Januari 12 mwakani.

Mbarawa ameeleza kuwa mamlaka zinazohusika na maji lazima zifanya kazi kibiashara hasa kwa kujituma na kutekeleza majukumu yao ili kuweza kuipeleka sekta hiyo mbele zaidi.

Mbarawa amesema kuwa kwa mwaka 2006 hadi mwaka 2016 miradi mbalimbali imetekelezwa na miradi mingi itatekelezwa  hadi kufikia mwaka 2021. Na ameeleza kuwa hadi sasa upatikaji wa maji katika miji ya Mikoa ni asilimia 75 na vijiji ni asilimia ni wa asilimia 59.8.

Pia Mbarawa amesema kuwa hadi sasa Miradi mikubwa na ya kitaifa 1801 imekamilika na mingine zaidi ya 500 bado inaendelea kutekelezwa ikiwemo Bagamoyo, Salasala, Bunyokwa na Kiwalani yenye thamani ya shilingi trioni 4.5 na miradi mingine katika Mikoa ya Arusha, Same/Mwanga na Tabora itatekelezwa na zaidi ya shilingi bilioni 400 zitatumika kuboresha huduma za maji.

Pia amesema kuwa mapatao ya mamlaka hiyo yaliyokusanywa yamepanda kutoka bilioni 8.2 mwezi June alipoteuliwa hadi kufikia bilioni 10.1 kwa sasa na amewataka wananchi kuamini Serikali na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ili kulipeleka taifa mbele zaidi.

Kuhusiana na usalama wa maji nchini Prof. Mbarawa amesema kuwa kuna maabara takribani 16 nchini na Mikoa iliyokosa maabara za Mikoa jirani katika upimaji wa maji na zoezi la upimaji wa maji hufanyika kila siku.

Aidha amewataka watanzania kutunza vyanzo vya maji na kutofanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji ili kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji na amewataka kuwa na imani na serikali kwa kuwa imejipanga  katika kuhakikisha kila mtanzania anapata maji safi na salama.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad