HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 3 December 2018

Muhimbili tawi la Mloganzila yaadhimisha siku ya Ukimwi Duniani kwa kutoa huduma ya upimaji wa afya bure

Muhimbili tawi la Mloganzila yaadhimisha siku ya Ukimwi Duniani kwa kutoa huduma ya upimaji wa afya bure. Mamia ya wananchi leo wamejitokeza kupima afya zao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambapo hospitali hiyo imefanya zoezi la upimaji bure pamoja na kutoa ushauri nasaha.

Akizungumza katika maadhimisho hayo ambayo yamefadhiliwa na kampuni ya HETERO Laboratories, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Tawi la Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema takwimu zinaonesha kuwa kila watanzania mia moja watu 4.7 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 kati yao wameathirika na Virusi vya Ukimwi na takribani watanzania 1.4 milioni wanaishi na Virusi vya Ukimwi.

Pia kwa mujibu wa Shirika la afya duniani -WHO-, watu milioni 37 duniani wanaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi huku vijana wakiendelea kuwa kundi lililoko hatarini zaidi kuambukizwa VVU hasa barani Afrika.

Akielezea kuhusu mafanikio ya utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Magandi amesema Muhimbili hutoa huduma za VVU katika kliniki zake za wagonjwa wa nje kila siku ambapo wagonjwa 3,534 wanahudumiwa, huku Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila ikihudumia takribani wagonjwa 70.

’Muhimbili imekua ikifanya maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kila mwaka na mwaka huu tumeamua kuwafikia watu wengi zaidi katika maeneo ya Mloganzila ili kupima hali za afya ikiwemo VVU pamoja na magonjwa mengine ya presha na kisukari’. amefafanua Dkt. Magandi.

Hata hivyo amesema changamoto iliyopo ni muitikio mdogo wa upimaji wa VVU katika vituo vya afya na kwamba Hospitali ya Taifa Muhimbili kama mdau katika vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi itaendelea kuhamasisha upimaji kila mara katika maeneo ya huduma za afya ndani na nje hospitali.

Shirika la kupambana na Ukimwi Duniani -UNAIDS- limeendelea kusaidia nchi mbalimbali duniani katika kupambana na hali ya VVU kwa malengo makuu matatu ambayo kufikia mwaka 2020 malengo hayo yawe yamefikiwa katika nchi zote.

Malengo hayo ni asilimia 90 ya watu wote wawe wanafahamu hali zao za maambukizi ya VVU, silimia 90 ya watu waliogundulika na maambukizi ya VVU wawe wanapata huduma za afya na ARV pia asilimia 90 ya watu waishio na VVU wanaotumia dawa za ARV wawe na kiwango cha chini cha virusi.

Kauli mbinu ya maadhimisho ya siku Ukimwi duniani mwaka huu ni ‘’ijue afya yako’’. 
 Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Tawi la Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akifungua maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambapo Muhimbili-tawi la Mloganzila imeadhimisha siku hiyo leo kwa kutoa huduma ya upimaji bure.
 Baadhi ya wananchi ambao wamejitokeza kwa ajili ya kupata huduma wakimsikiliza Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo.
 Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya kuambukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Amina Mgunja akitoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Ukimwi.
 Wauguzi wa Muhimbili wakiendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani Pamela Kaaya (kushoto) akimpatia huduma mmoja wa wateja ambaye amejitokeza kwa ajili ya kupata huduma za afya katika maadhimisho hayo.
 Wananchi wakisubiri kupata huduma ya upimaji katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo yamefanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Tawi la Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akiwa katika picha ya pamoja na watoa huduma katika maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad