HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 13 December 2018

Mbunge wa Njombe mjini Edward mwalongo akikagua ujenzi wa miradi mbalimbali jimboni kwake

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Mfuko wa Jimbo iliyofanywa kwa lengo la kukagua na kupitisha miradi itakayosaidiwa na Mfuko huo, Mbunge wa Jimbo la Njombe Kusini Edward Mwalongo amesema kuwa kiasi cha shilingi milioni 40 kitatumika kununulia vifaa vya ujenzi kulingana na mahitaji ya mradi husika na vitagawiwa kwenye Kata 13 za jimbo hilo ili kuweza kuchochea na kuchangia kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mwalongo amesema kuwa vipaumbele vya Mfuko wa Jimbo ni kusaidia miradi ya afya, elimu pamoja na utawala mara baada ya kufanyika upembuzi yakinifu na kubaini mahitaji ya vifaa kwenye miradi iliyoibuliwa na wananchi na ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 mfuko wa jimbo umefanikiwa kufanya jambo la upekee katika sekta ya elimu tofauti na vipindi vingine jambo ambalo limepokelewa kwa furaha na wanafunzi na uongozi wa Ruhuji shule ya Msingi.

“Kitu cha pekee ambacho Mfuko wa Jimbo umefanya katika mwaka huu wa fedha 2018/2019 ni kusaidia ujenzi wa jiko maalumu katika Shule ya Msingi Ruhuji ambalo litakua linatumia kuni kidogo, na rafiki wa Mazingira lakini pia ununuzi wa sufuria aina ya “Stainless steel”ambayo ni imara na haipati kutu na itatumika kwa muda mrefu. Hii itaonesha njia kwa Shule nyingine za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Njombe kwamba jiko bora na sufuria bora liko Ruhuji Shule ya Msingi na wanaweza kufika pale kujifunza.”Alisema Mbunge wa Jimbo la Njombe Kusini Mhe. Mwalongo.

Sambamba na hilo Mwalongo amewaomba  Waheshimiwa Madiwani kutambua kwamba Mfuko wa Jimbo upo kwa ajili ya kuchochea maendeleo na kigezo kimoja wapo ni kwamba lazima wao wenyewe kwenye maeneo yao wawe wameanza.

“Mfuko wa Jimbo hauji kuwasha maendeleo unakuja kuchochea, vipo vijiji kama vitano kwenye Jimbo letu ambavyo havijawahi kupata ruzuku ya Mfuko wa Jimbo kwa kipindi chote hii ni kwa sababu maeneo yale hayana mradi wa aina yoyote. Niwaombe vijiji hivyo wananchi kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani kuibua miradi na waanze utekelezaji na itakapofikia kipindi cha ufadhili wa mfuko wa Jimbo tutaikagua na ikikidhi vigezo tutawapatia vifaa vya ujenzi ili miradi hiyo ikamilike na ianze kutumika kwa manufaa ya wananchi kwa ujumla” Mwalongo alisema

Kwa upande wake Daniela Msemwa ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Makowo Kata ya Makowo amesema kuwa wanashukuru uwepo wa Mfuko wa Jimbo na anampongeza Mhe. Mbunge wa Jimbo la Njombe Kusini kwa jinsi anavyosimamia mfuko huo kwani Mfuko huo umekuwa ukichochea maendeleo katika Kata yao na umewahamasisha wananchi wengi kujitolea kuchangia shughuli za maendeleo kwenye Kata hiyo.

Kamati hiyo pia imeshauri ni vyema Wataalamu wa Halmashauri kuwa na mawasiliano ya karibu na Wananchi ili kuweza kutoa ushauri wa kitaalamu ikiwemo matumizi sahihi ya viwango vya ujenzi na michoro ili kuepuka lawama na uharibifu wa rasilimali za wananchi.

Mfuko wa Jimbo ulifanikiwa kutembelea miradi 40 katika Kata 13 zilizopo kwenye Halmashauri ya Mji Njombe na imefanikiwa kuipitisha miradi 19 katika kata hizo ambazo zitapatiwa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Tsh. Milioni 38 na Milioni mbili zitatumika kwa ajili ya kuchangia mradi wa ujenzi wa vyoo vya kisasa vya wasichana katika shule ya Msingi Mpechi mradi ambao unatekelezwa na Umoja wa Wabunge Wanawake katika kila Jimbo Nchi nzima.
Mbunge wa Njombe mjini Edward Mwalongo(wa kwanza kulia) akikagua ujenzi wa miradi mbalimbali wakati wa ziara ya Kamati ya Mfuko wa Jimbo iliyofanywa kwa lengo la kukagua na kupitisha miradi jimboni kwake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad