
Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
KESI ya uchochezi dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko na wenzao saba inayounguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepigwa kalenda hadi Januari 3 mwakani.
Mbowe na Matiko wataendelea kusota mahabusu hadi Januari 3 baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusimamisha usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na washitakiwa hao kupinga maamuzi ya Mahakama ya Kisutu ya kuwafutia dhamana.

Hata hivyo wakili Faraja Mangula amedai kuwa wakili wa washtakiwa hao Peter Kibatala na Sheck Mfinanga wamepata dharura na kuiomba mahakama ipange Januari 4, mwakani.
Akijibu hoja hiyo wakili Saimoni alidai wanaiachia mahakama ipange tarehe itakayoona inafaa kusikilizwa kwa shauri hilo. Hakimu Mashauri amesema kuwa Januari 4 mwakani atakuwa na kazi nyingine hivyo amehairisha kesi hiyo hadi Januari 3 mwakani. Baada ya kuelezwa hayo Mbowe na Matiko waliwatakia wafuasi wao heri ya sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wakiamini hawawezi kutoka gerezani kwa kipindi hiki.

Washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, jijini Dar es Salam.
No comments:
Post a Comment