HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 11, 2018

JAJI MKUU ATOA WITO KWA VIONGOZI KUELIMISHA WANANCHI TARATIBU ZA UPATIKANAJI WA HAKI

Na Lydia Churi- Mahakama Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa viongozi wa Mahakama, Serikali pamoja na Dini kuwaelimisha wananchi taratibu mbalimbali za upatikanaji wa haki. 
Akizungumza na wakuu wa wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma leo, Jaji Mkuu amesema wananchi wengi hawafahamu taratibu za upatikanaji wa haki hivyo viongozi hao wanao wajibu wa kuwaelimisha kwa lugha ya upole wanapofika kwenye maeneo yao ya kazi.
Alisema kutokana na kutokufahamu taratibu za upatikanaji wa haki, wananchi wengine wamejikuta wakipoteza haki zao na wengine kutumia muda mwingi kushughulika na kesi ambazo thamani yake hailingani na muda na mali iliyotumika. 
“Wengine hudhani kupata haki ni kushinda kesi hawajui kwenye kesi kuna kushinda na kushindwa, dhana hii ndiyo inayoibua migogoro hivyo wananchi hawana budi kuelimishwa kuwa haki kwa aliyeshindwa ni kukata rufaa”, alisema Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania imejiwekea vigezo ili kuhakikisha inaboresha huduma zake na wananchi wanapata haki kwa wakati. 
Vigezo hivyo ni pamoja na kuhakikisha kesi inamalizika ndani ya miaka miwili kwenye Mahakama Kuu, miezi 12 kwenye Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za Wilaya  na miezi sita kwenye Mahakama za Mwanzo.
Kigezo kingine ni mapambano dhidi ya rushwa ambapo alisema Mahakama imesambaza nchi nzima mabango yenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa, simu za mikononi na pia imewapatia watumishi wake wote vitambulisho.
Alisema Mahakama inaimarisha vitengo vya usuluhishi kikiwemo kitengo cha usuluhishi na mabaraza ya kata hasa kwenye maeneo  yasiyokuwa na Mahakama za Mwanzo. 
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama pia hutoa nakala za hukumu bure na kuhakikisha nakala hizo zinatoka ndani ya siku 21, kupatikana kwa mienedo ya kesi ndani ya siku 30 ili kuwafikia wananchi na kutoa haki kwa wakati. 
Akizungumzia ushirikiano na mihimili mingine, Jaji Mkuu alisema mihimili yote ya dola inategemeana hivyo Mahakama haina budi kushirikiana ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Naye Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga akimkaribisha Jaji Mkuu wilayani kwake alisema wilaya yake itaendeleza ushirikiano kati yake na Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania ameanza ziara ya siku mbili katika mkoa wa Dodoma ambapo leo ametembelea wilaya ya Chemba pamoja na Mahakama ya wilaya ya Kondoa na kukagua shughuli za Mahakama.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad