HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 19 November 2018

WAZIRI WA FEDHA AHIMIZA TRA KUTENGENEZA WALIPA KODI NCHINI

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji ameitaka Mamlaka ya mapato nchini ( TRA) kuwa na mpango wa kuwatengeneza walipakodi na sio kutegemea walipakodi waliozoeleka pekee kwa kuwa wananchi wana utayari wa kulipa kodi ila hawafikiwi na mamlaka hiyo.

Akihutubia na kutunuku vyeti kwa wanafunzi 360 wa ngazi za vyeti, stashahada na shahada  katika mahafali ya kumi na moja ya chuo cha kodi  jijini Dar es Salaam Dkt. Kijaji amesema kuwa maendeleo endelevu yatafikiwa kwa kuangalia na kuwafuata walipa kodi na sio kukaa maofisini, na ameitaka mamlaka hiyo kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi hasa za majengo na kusema kuwa wananchi wapo tayari kulipa kodi hizo ila hawafikiwi na wataalamu kutoka katika mamlaka hizo.

Aidha amesema kuwa kupitia bodi ya mikopo wataendelea kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha za mikopo ili kuwawezesha wanafunzi wengi wakiwemo wanaosomea masuala ya taaluma ya kodi kupata fedha za kulipia masomo yao.

Pia Kijaji amewataka wahitimu  hao kutumia vizuri kofia walizopewa na chuo hicho na kuwa mabalozi wazuri wa chuo cha kodi na kuisaidia Serikali kutoa elimu na kukusanya kodi ili kuweza kufikia azma ya Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Dkt. John Magufuli ya kufikia uchumi wa kati.

Kwa upande wake Kamshina mkuu wa mamlaka ya mapato nchini Charles Kichere amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kutumia vyeti vyao vizuri katika kuleta maendeleo ya taifa.

Kichere amesema kuwa  mamlaka hiyo inahakikisha elimu ya kodi inasambaa nchi nzima  kwa wadau  na taasisi kuhusiana na ulipaji wa kodi kwa hiari.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha kodi Profesa Isaya Jairo amesema kuwa zaidi ya watumishi 4449 wa mamlaka ya mapato nchini ndani ya miaka mitano wamepata elimu kuhusiana na masuala ya kodi na forodha na amesema kuwa udahili wa wanafunzi katika chuo hicho umekuwa ukiongezeka kila mwaka na hiyo ni kutokana na upekee na ubora wa elimu inayotolewa chuoni hapo.

Jairo amesema kuwa chuo hicho kinashirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi  hasa zile zinazojihusisha na masuala ya forodha katika kuhakikisha wanaboresha sekta hiyo kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad