HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 19, 2018

WAZIRI MKUU AWATAKA WANANCHI WAJENGE MABWENI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi kwenye Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa washirikiane kujenga mabweni katika shule ya sekondari Mnacho ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembelea umbali mrefu kwenda shuleni hapo.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 19, 2018) wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni, ambalo ujenzi wake unagharimu sh. milioni 92.4 ikiwa ni mchango uliotolewa na wadau wa elimu.
“Bweni hili likikamilika litawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja shuleni hususani wanaoishi vijiji vya mbali kwa sababu wataishi hapa, jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wa watoto wetu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio katika Kata hiyo na za jirani washirikiane na kuanzisha mradi wa ujenzi wa mabweni mengine kwa kuwa hilo moja lililojengwa na wadau halitoshi kulingana na idadi ya wanafunzi.
Amesema yeye yuko tayari kuendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao yote ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata yao, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati ya Serikali ya kuboresha huduma za jamii inatimia.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi hao washirikiane na walimu kufuatilia maendeleo ya taaluma kwa watoto wao shuleni na kujiridhisha kama wanafanya vizuri darasani na iwapo watabaini changamoto waweze kuzitatua kwa pamoja.  
Akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni hilo, Mkuu wa shule ya sekondari Mnacho, Mwalimu David Mwakalobo amesemma ujenzi wa bweni hilo lenye uwezo kulaza wanafunzi 80 ulianza Septemba 19, 2018 na unatarajiwa kukamilika Januari, 2019.
“Kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo shuleni bweni hili litakidhi mahitaji ya kuwalaza wanafunzi wa kike tu. Tunaendelea kuwaomba wahisani waendelee kutusaidia ili tupate bweni lingine kwa ajili ya kuwalaza wanafunzi wa kiume.”
Mwalimu Mwakalobo amesema iwapo watafanikiwa kuwa na mabweni ya kuwalaza wanafunzi wote 334 shuleni hapo yatawasaidia katika kutatua changamoto ya utoro na mdondoko wa kitaaluma kwa wanafunzi kwa sababu wengi wanatoka mbali.
Pia mradi wa ujenzi wa mabweni utasaidia walimu kuwa karibu na wanafunzi wakati wote, hivyo kupata muda mwingi wa kuwasaidia wanafunzi kimasomo kwa sababu watakuwa wanaishi shuleni. “Mradi huu pia utapunguza wanafunzi wengi wa kike kupata ujauzito.”
Ameongeza kuwa uwepo wa mabweni shuleni hapo utaongeza ari ya wanafunzi kupenda shule tofauti na hali ilivyo sasa kwa sababu wengi wanalazimika kutembea muda mrefu kwa kuwa wanatoka vijiji vya mbali, jambo linalowafanya wasipende shule.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Mnacho wilayani Ruangwa, David Mwakalobo wakati alipokagua ujenzi wa bweni hilo Novemba 19, 2018 . Kulia kwake ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandirwa. (Picha na Ofisi  ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kulaza wanfunzi 80  katika shule ya Sekondari ya Mnacho wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Shule hiyo,  David Mwakalobo.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waganga na Wanguzi wa Zahanati ya Nandagala wilayani Ruangwa kabla ya kukagua ujenzi wa majengo ya Zahanati hiyo Novemba 19, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsalimia mtoto Hamza Abdulrazak aliyepelekwa na Mama yake Mzazi, Mariam Liwena  (wapili kushoto) katika Zahanati ya Nandagala wilayani Ruangwa kwa matibabu, Novemba 19, 2018. Watatu kushoto ni   Ajira Mpoka na mwanae Naifat Arifa. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Zahanati ya Nandagala wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018. Kushoto ni Mganga Mfawidhi wa Zahanati  hiyo, Abubakar Abbas Rugwa. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Zahanati ya Nandagala wilayani Ruangwa Novemba 19, 2018. Kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandirwa, kushoto ni Mganga Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Dkt.  Mahela Njile na kushoto ni Mganga  Mfawidhi wa Zahanati hiyo, Abubakar Abbas Rugwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad