HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 29, 2018

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO 5 KWA KAMATI YA USIMAMIZI WA MENEJIMENTI YA MAAFA YA MKOA WA DAR ES SALAAM

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amefanya ziara ya siku moja mkoani Dar es salaam, lengo la ziara hiyo ni kukagua miundo mbinu ya kukabiliana na maafa ya mafuriko pamoja na kutaka kujua mikakati ya kamati ya Usimamizi wa menejimenti ya maafa mkoani humo ya kukabiliana na maafa hayo.

Katika ziara hiyo Waziri Mhagama emetembelea wilaya zote za mkoa wa Dar es salaam hususan katika maeneo ambayo mkoa huo umeboresha miundo mbinu ya kukabiliana na maafa ya mafuriko. Maeneo hayo ni Jangwani, Mto Mbezi, Mto Ng’ombe, Mto Bungoni na mfereji wa Mtoni kwa Azizi Ally. Pamoja na kuridhishwa na jitihada zilizofanywa na mkoa wa Dar es salaam za kuboresha miundombinu ya kukabiliana na maafa ya mafuriko, pia na mikakati ya kukabiliana na maafa hayo waliyomueleza, Waziri Mhagama ametoa maagizo 5 kwa kamati ya Usimamizi wa menejimenti ya maafa ya mkoa huo kuyatekeleza  ili menejimenti ya maafa ya mafuriko mkaoni Dares salaam iwe endelevu.

“Nimeridhishwa na juhudi zilizofanywa na serikali kuu chini ya uongozi wa Dkt.Joh Pombe Magufuli za kuboresha miundo mbinu ya kakabiliana na maafa ya mafuriko, na nimeona jinsi serikali ya ngazi ya mkoa na wilaya zote zinavyo jitahidi kujenga uwezo   wa kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa. Pamoja na jitihada hizo ninge penda kuishauri  na kuielekeza kamati na Mkuu wa mkoa ayasimamie maelekezo yangu.” Amesisitiza  Mhagama
Mhagama ameiagiza Kamati ya Usimamizi wa menejimenti ya maafa kusimamia suala la uharibifu wa mazingira hususani maeneo ya mito na mabondeni kwa mujibu wa sheria ya menejimenti ya maafa ya mwaka 2015. Aidha alifafanua kuwa Maafa mengi ya mafuriko mkoani humo yanatokana na uharibifu wa mazingira unaochangiwa na  ujenzi  katika maeneno yasiyo stahili kama kingo za mito na mabondeni hali ambayo huzuia maji kutiririka na kusababisha mafuriko.

Aidha Mhagama ameitaka kamati hiyo  kusimamia suala la usafi wa mitaro, mifereji na mito iliyopo  jijini  Dares salaam, ambayo hujaa maji wakati wa msimu wa mvua kutokana  na uchafu na takataka zilizotupwa katika mifereji na mitaro hiyo hali ambayo husababisha maji kushindwa kutirirka kuelekea baharini na hatimaye mitaro hiyo hujaa na kusababisha mafuriko. Ameitaka kamati hiyo kuwasiliana na sekta nyingine zenye miundmbinu katika mitaro na mifereji inayojengwa na kuondoa miundo mbinu hiyo ili uboreshaji wa miundo mbinu hiyo kuwa wa ufanisi. Mhagama alibainisha kuwa Mkoa umefanya  juhudi nzuri za kujenga mitaro na mifereji lakini ndani ya  miundo mbinu hiyo  kuna miundombinu mingine kama vile mabomba ya  maji safi,  hivyo,  sekta nyingine husika hazina budi kushrikishwa na kuhakikisha miundo mbinu hiyo inatolewa ili kulifanya zoezi la kuboresha miundombinu ya maafa ya mafuriko linakuwa bora na ufanisi.

Kamati imetakiwa kuhakikisha miradi yote inayolenga kuboresha miundombinu ya kukabiliana na maafa ya mafuriko ndani ya mkoa wa Dar es salaam inashirikiana katika hatua ya kupanga utekelezaji wake. Mhagama amefafanua kuwa Mkoa una miradi mingi ya kuboresha miundo mbinu ya kukabiliana na maafa hivyo ni vyema miradi hiyo ikae pamoja ili kujua ni namna gani ya kutekeleza malengo yake hususani kujua miundo mbinu husika inawekwa wapi bila kuathiri utekelezaji wa mradi mwingine. Mhe.Mhagama ameitaka kamati kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya sheria ya menejimenti ya maafa ya mwaka 2015. Amebainisha kuwa kila mmoja katika jamii analojukumu la kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa, hivyo jamii ikiwa na elimu ya kutosha juu ya menejimenti ya maafa hususani ya mafuriko jamii haitapata athari kubwa za uharibifu wa mali na vifo vitokanavyo  na maafa ya mafuriko.

 Awali akieleza mikakati iliyopo ya kukabibiliana na maafa katika mkoa wa Dar es salaam, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alifafanua kuwa mkoa wa Dar es salam umekuwa ukitumia fedha nyingi wakati wa kurejesha hali ya miundo mbinu iliyoathirika kutokana na maafa ya mafuriko ambapo kwa mwaka 2011, kiasi cha shilingi bilioni Nne na nusu kilitumika kurejesha hali ya miundo mbinu ya barabara iliyoharibika.
“Mkoa wa Dar es salaam tuna mito mikubwa saba ambayo inatiririsha maji  kuelekea baharini, na mito midogo midogo mingi, sisi kama mkoa tumejipanga kuhakikisha mito hiyo ambayo hujaa maji na kusababisha maafa ya mafuriko tunaidhibiti. Kupitia Benki ya Dunia tunao mpango wa kuchukua picha za anga la mkoa wa Dar es salaam, lengo ni kujua nyumba zilizo kando ya mito hiyo  na idadi ya mito na kujipanga jinsi ya kuhakikisha kuwa haileti athari ya mafuriko”amesema  Makonda.

Naye mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Menejimenti ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa mujibu wa sheria ya maafa ya menejimenti ya maafa mwaka 2015, Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es Salaam, alimhakikishia Waziri Mhagama kutelekeleza maagizo hayo kwa wakati kwa kuwa tayari kamati ya Usimamizi wa menejimenti wa maafa ya mkoa imesimamaia uundwaji wa kamati za Usimamizi wa menejimenti ya maafa katika Halmashauri zake tano hai itakayo saidia ufuatiliaji wa masuaa ya maafa mkoani humo.
Katika ziara hiyo Waziri Mhagama aliambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa. Faustin  Kamuzora, Mkurugenzi wa Idara ya uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, Mkuu wa wila ya  Ilala,  Temeke, na Kinondoni pamoja na wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Menejimenti ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliye kuwa akimueleza juu ya ujenzi wa mfereji wa mto Ngo’mbe, wakati wa ziara yake  ya kukagua miundo mbinu ya kukabili maafa ya mafuriko mkoani Dar es Salaam.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza, Bibi, Nuru Damson, mkazi wa Dar es Salaam, aliye kuwa akimueleza  jinsi ujenzi wa mfereji wa mto Ngo’mbe, ulivyowasaidia kutopata athari za maafa ya mafuriko wakati wa ziara yake  ya kukagua miundo mbinu ya kukabili maafa ya mafuriko mkoani Dar es Salaam. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akioneshwa ujenzi wa miundombinu ya kukabili maafa ya mafuriko mkoani Dar es saaam na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakati wa ziara yake  ya kukagua miundo mbinu hiyo mkoani humo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad