HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 14 November 2018

"UCHOVU NI SABABU INAYOPELEKEA AJALI ZA BARABARANI" -- DKT. MPOKI

Na WAMJW, Dar es Salaam.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa moja ya sababu za ajali barabarani, ni uchovu wa madereva.

Dkt. Mpoki ameyasema Novemba 13, 2018 wakati wa kufungua mafunzo ya watoa huduma za tiba, uokoaji na usafirishaji wa majeruhi wa ajali na wagonjwa wenye dharura mbalimbali nje ya Hospitali nchini.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Mpoki amelitaka jeshi la Polisi nchini kuangalia namna ya kuweka utaratibu wa madereva kubadilishana kwani suala la uchovu linachangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani.

Aidha, akitolea mfano suala la uchovu, dereva kutoka Mwanza au Bukoba kwenda Dar es Salaam, basi ashuke Singida ili aingie dereva mwingine kumalizia safari na hiyo itasaidia kuepusha ajali.

“Tumemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi atusaidie kama mchango wa Polisi katika kupunguza ajali kwa kuhakikisha kwamba wanaweka utaratibu wa madereva wanaendesha kwa muda maalum. Kuliko ilivyo sasa madereva wanaweza kuendesha siku nzima, Hivyo wanakuwa wachovu na kuchangia kwa kiasi kikubwa sana ajali mbalimbali barabarani” amesema Dkt. Mpoki.

Hata hivyo ameeleza kuwa, mpango huo ni hatua ya kwanza ambayo Serikali imewekeza kuingilia kati pale watu wanapokuwa wameumia, ambapo huko nyuma maisha ya watu wengi yalikuwa yakipotea kwa sababu vifaa vilikuwa vinachelewa sana kufika mahali tukio na hivyo kushirikiana na Benki ya dunia kwa kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya uwekezaji na shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za wataalam.

“Katika fani ya tiba, Tunazungumzia saa ya kwanza ni saa muhimu sana kusaidia mtu aliyepata changamoto ya ajali. Hawa watakuwa chachu ya kusaidia kati ya wale waliopata mafunzo.” Amesema Dkt. Mpoki

Dkt. Mpoki ameongeza kuwa katika afua hiyo,itakuwa na vituo maalum   vyenye miundombinu ya kutoa huduma hizo ambapo awamu ya kwanza itaanzia Dar e Salaam hadi Ruaha Mbuyuni na kwa kila kituo kutakuwa na gari la kubebea wagonjwa, vifaa vya zima moto na kuweka utaratibu wa kusafirisha majeruhi kwa kushirikiana  majeshi yakiwemo la Jeshi la Wananchi (JWTZ), Polisi, Zimamoto pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD).

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma (MUHAS), Profesa Appolenary Kamuhabwa  amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwani  kutakuwa na mfumo thabiti wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura watokanao na ajali na  ni hatua muhimu  kwani bila afya bora, wananchi hawawezi kutumikia nchi hususani  ajenda ya Serikali ya  viwanda.

Profesa Kamuhabwa amesema katika mpanguo huo, utakuwa na vituo mbalimbali vya Afya vitakavyokuwa vikitoa huduma za dharura ikiwemo: Vituo vya Afya vya Kimara (Dar es Salaam), Tumbi,  Chalinze (Pwani), Mikese, St, Kizito, Doma-Mikumi (Morogoro) na Ruaha Mbuyuni (Iringa).
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya  akizungumzawakati wa  kufungua mafunzo ya watoa huduma za tiba, uokoaji na usafirishaji wa majeruhi wa ajali na wagonjwa wenye dharura mbalimbali nje ya Hospitali nchini  jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa MMG)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akizindua kitabu cha mafunzo ya watoa huduma za tiba, uokoaji na usafirishaji wa majeruhi  wa ajali na wagonjwa wenye dharura mbalimbali nje  ya hospitali nchini Tanzania
 Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma (MUHAS), Profesa Appolenary Kamuhabwa akizungumza machache  wakati wa ukufungua wa mafunzo ya watoa huduma za tiba  jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi  wa idara ya dharura hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt .Juma Mfinanga akipokea  kitabu hicho  cha mafunzo  kutoka kwa Katibu Mkuu  Dkt. Mpoki  Mara baada ya kukizindua
Picha ya Pamoja

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad