HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 21 November 2018

PROFESA MBARAWA ASHIRIKI UPANDAJI WA MITI PEMBEZONI MWA MTO KIZINGA

*Awataka wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya vizazi vijavyo.
*Mito zaidi ya 10,000 kupandwa Mto Mzinga, kampeni kuendelea hadi Mto Ruvu 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa eneo la Mtoni Mashine ya maji na kuwataka kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu  na kuacha kulima pembezoni mwa mito.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa amewaomba wananchi kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu  na kuacha kulima pembezoni mwa mito.

Ameyasema hayo leo wakati wa upandaji miti aina ya Mitomondo pembezoni mwa mto Kizinga akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja.

 Akizungumza na wananchi wa eneo la Mtoni Mashine ya maji, Profesa Mbarawa amesema wananchi wanatakiwa kulinda vyanzo vya maji ili wapate majisafi na salama kwa manufaa yaona vizazi vijavyo.

Amesema, amehakikisha wanaanza kampeni maalumu kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji, na wakivilinda vizazi vijavyo vitapata maji safi na salama na serikali watapoteza pesa nyingi iwapo wananchi wataharibu vyanzo hivyo.

Amesema Serikali inatumia pesa nyingi kujenva  miundo mbinu ya maji na iwapo vyanzo vikiharibikiwa na basi haitaweza kufanya kazi ya kusambaza maji safi na salama.

"Lazima tusimamie sheria, serikali inawekeza hela nyingi sana katika kujenga miundo mbinu na kampeni hii imeanzia  Mtwara, Ruvuma na Dar es salaam na hii itaendelea nchi nzima,"amesema Mbarawa.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva amesema mtambo huu wa maji wa Mtoni ulijengwa mwaka 1949 ukihudumia mkoa mzima wa Dar es Salaam.

Lyaniva amewasihi wananchi wanaoishi pembezoni mwa mto Mzinga kuacha kulima kwani kufanya hivyo wanasababisha maji kukauka na kusababisha ukosefu wa maji.

"Nilianza na nitaendelea kupanda miti pembezoni mwa vyanzo vya maji, suala hili nimeliwekea kipaumbele kwani maji ni muhimu na wananchi wanahitaji maji," amesema Lyaniva.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Cyprian Luhemeja amesema kuna changamoto kubwa ya uharibifu wa vyanzo vya maji kwa wananchi kulima pembezoni mwa mto na wameanza kampeni hii ya kupanda miti kwenye maeneo yote.

Luhemeja amesema, wameanza kupanda miti katika chanzo cha mto Kizinga na watafuata kwenye mto Ruvu ili kulinda vyanzo hivyo kwa kupanda miti ya mitomondo inayoweza kuhimili ukame kwa muda mrefu.

Miti takribani 10,000 itapandwa kwenye chanzo cha mto Kizinga kwa kipindi tofauti na Desemba 9 mwaka huu watashirikiana na wananchi wapenda maendeleo  na wafanyakazi wa DAWASA kupanda pindi kwenye chanzo cha mto Ruvu.

Chanzo cha mto Kizinga kinazalisha maji lita Milioni tisa kwa siku maji yanayosambazwa kwenye maeneo ya Mtoni, Kurasini, Mtoni Kijichi na Chang'ombe.
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akipanda mti kwenye Chanzo cha Mto Kizinga ikiwa ni kampeni ya Upandaji miti pembenzoni mwa vyanzo vya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva akiwa anapamba mtikwenye Chanzo cha Mto Kizinga ikiwa ni kampeni ya Upandaji miti pembenzoni mwa vyanzo vya maji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam ( DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akipanda mti kwenye Chanzo cha Mto Kizinga ikiwa ni kampeni ya Upandaji miti pembenzoni mwa vyanzo vya maji

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad