HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 26 November 2018

MKUTANO WA 12 WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI KUANZA JUMATANO

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar 
Mkutano wa 12 wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza siku ya Jumatano tarehe 28 Novemba 2018 katika Ukumbi wa Baraza hilo Chukwani. Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari Ofisini kwake, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem alisema jumla ya maswali 123 yameratibiwa kwa ajili ya kujibiwa kwenye mkutano huo.

Alisema Miswada mitatu ya sheria iliyowasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa mwezi Septemba itasomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa katika mkutano huo. Aliitaja miswada hiyo kuwa ni mswada wa Sheria ya kuweka masharti yanayosimamia Utoaji wa Huduma za msaada wa Kisheria, kurahisisha upatikanaji wa haki na kuweka masharti mengine yanayohusiana na hayo.

Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya ukuzaji na kulinda vitegau uchumi Zanzibar Nam. 11 ya mwaka 2004 na kutunga sheria ya Mamlaka ya Ukuzaji na kulinda vitega uchumi Zanzibar. Katibu wa Baraza Raya Issa Msellem alitaja mswada mwengine kuwa ni mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Vyama vya Ushirika Nam. 4 ya mwaka 1986 na kutunga Sheria ya vyama vya Ushirika Zanzibar ya mwaka 2018 ambayo inaweka utaratibu wa uundaji na uendeshaji wa vyama vya Ushirika na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Alieleza kuwa Katika Mkutano huo taarifa ya Serikali kuhusu hoja ya Mjumbe Jaku Hashim Ayoub ya kutoa Azimio la kuitaka Serikali kuja na Mkakati unaotekelezeka kwa kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la mwani itatolewa. Hoja nyengine ni ya Mjumbe kuhusu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka viti maalum vya wanawake kufaidika na fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo na hoja ya Mjumbe kuhusu kuimarisha tathmini na ufuatiliaji wa miradi Zanzibar zitawasilishwa. 
 Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem akitoa taarifa  kwa Waandishi wa Habari kuhusu kuanza Mkutano wa 12 wa Baraza la Tisa la Wawakilishi (kulia) Mkuu wa Idara ya shughuli za Baraza Mussa kombo na Mkuu wa Idara ya Utawala Amour Mohd.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (hayupo pichani) alipokuwa akitoa taarifa ya kuanza Mkutano wa 12 wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Ofisini kwake Chukwani. Picha na Ramadhani Ali – Maelezo.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad