MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kutumikia kifungo cha miaka 2 jela ama kulipa faini ya Milioni 9.3 wafanyakazi watatu wa Kampuni ya Jiangxi International (T) Investment Ltd baada ya kukiri makosa ya kushindwa kuchukua tathmini ya uaribifu wa mazingira.
Washtakiwa hao ni Injinia Xia Yanan (26), Chen Jinchuan (31) raia wa China na Mtala Habibu (29) fundi umeme raia wa Tanzania.
Hukumu hiyo imetolewa leo Novemba 7, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa Serikali Nassoro Katuga kuwasomea washtakiwa makosa yao na kukiri.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shaidi amesema kutokana na washtakiwa kukiri makosa yao anawahukumu kila mmoja kulipa faini ya Shilingi Milioni Tatu na laki moja kwa makosa yote mawili ama kwenda kutumikia kifungo cha miaka miaka 2 gerezani.

Pia kosa la pili la kutotii amri halali ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wamehukumiwa kulipa faini ya Shilingi Laki Moja ama jela miaka 2 kila mmoja.
Washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha na kuachiwa huru.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka kosa la kushindwa kuchukua tathmini ya Uaribifu wa mazingira, wamelitenda kati ya January na August 28,2018 maeneo ya Regent Estate Kinondoni ambapo waliendeleza ujenzi bila kuchukua tahadhari ya mazingira kutoka NEMC.
Pia katika kosa la kutotii amri (NEMC), wamelitenda August 25,2018 maeneo ya Regent Estate Kinondoni Dar es Salaam, ambapo walishindwa kutii amri halali kupitia barua ya NEMC ya kusimamisha ujenzi.
No comments:
Post a Comment