Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende, kuhusu kuifanyia matengenezo barabara ya Majimoto-Inyonga yenye urefu wa KM 130 kwa kiwango cha changarawe, mkoani humo.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende, akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati), kuhusu ukamilikaji wa Daraja la Kavuu linalounganisha Wilaya ya Mlele na Mpwimbwe mkoani humo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akitoka kukagua kingo za Daraja la Kavuu linalounganisha Wilaya ya Mlele na Mpwimbwe mkoani Katavi. Daraja hilo limekamilika na limeanza kutumika kwa magari yasiozidi tani 30.
Muonekano wa Daraja la Kavuu lenye urefu wa mita 85.344linalounganisha Wilaya ya Mlele na Mpwimbwe mkoani Katavi. Daraja hilo limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.718.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, amekagua daraja la kavuu lililokamilika kujengwa katika barabara ya Majimoto-Inyonga yenye urefu wa KM 130.
Katibu Mkuu amesema kuwa lengo la ujenzi wa daraja hilo ni kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji kwa mkoa wa Katavi. Daraja hilo lenye urefu wa mita 85.344 limegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 kwa gharama ya kiasi cha shilingi bilioni 2.718
Mhandisi Nyamhanga ameongeza kuwa kwa sasa daraja hilo limeanza kutumika kwa magari yasiozidi tani 30 na hivyo kufanya kupunguza urefu wa KM 135 endapo mwanachi hatapitia Mpanda. "Nimeridhishwa kwa kukamilika kwa daraja hili kwani ilikuwa ni kero kwa wananchi wa wilaya hizi kuzunguka umbali mrefu na gharama za usafiri kupanda", amesema Mhandisi Nyamhanga.
Aidha, amewataka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuendelea kuifanyia matengenezo barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ambacho itarahisisha kupitika kwa wakati wote. Naye Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende, amemueleza Katibu huyo kuwa kazi za uwekaji wa kitanda cha chuma katika daraja hilo ulifanywa pamoja na wahandisi wa ndani ikiwa ni lengo la kuongeza uwezo na uelewa katika ujenzi wa madaraja yanayotumika hasa nyakati za dharura.
Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Nyamhanga, yupo katika ziara ya kikazi mkoani Katavi ikiwa ni lengo la kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na sekta yake hususani barabara, madaraja na kiwanja cha ndege.
No comments:
Post a Comment