HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 30 November 2018

JUHUDI ZA HKMU ZAPONGEZWA, WASHAURIWA KUONGEZA IDADI YA WADAHILIWA

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
KONGAMANO la kwanza la kitaaluma la Chuo kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki limefanyika leo kwa kuwakutanisha wataalamu na baadhi ya wanafunzi waliosoma katika chuo hicho.

Akifungua kongamano hilo Katibu mkuu wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amepongeza juhudi zinazofanya na taasisi hiyo katika kuboresha sekta ya afya na anafurahi kuona wanafunzi bora wanatoka katika chuo hicho ambacho aliwahi kufundisha wakifanya kazi ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikifanya vizuri na mchango wao katika sekta ya afya unaonekana na wao kama Wizara wapo bega kwa bega katika kuhakikisha wanaimarisha vyema sekta ya afya nchini.

Dkt. Mpoki amewataka wahitimu na wanafunzi kujiunga katika taasisi mbalimbali za afya na ameshauri kuwa kongomano hilo liwe endelevu katika kuimarisha  na kufikia malengo waliyojiwekea ambayo yataonesha uimara na ubora wa taasisi hiyo.

Aidha amesema kuwa taasisi hiyo lazima ijijenge ili kuweza kuendelea kudahili wanafunzi wengi bora na hilo litafanikiwa kama wahitimu watafanya kazi zenye thamani za kutangaza taasisi hiyo.

Kwa upande wake Rais wa kongamano hilo Dkt. Leonard Malasa amesema kuwa kongamano hilo ni la kihistoria kuwahi kufanyika na zaidi ya wahitimu 1000 wa sekta ya afya wamehitimu tangu chuo hicho kimeanzishwa 1997.

Malasa amesema kuwa wataalamu waliosoma katika chuo hicho kutoka ndani na nje ya nchi wamejumuika pamoja katika kujadili na kueleza uzoefu na mafanikio yao waliyofikia kama vile kuanzisha hospitali binafsi, taasisi na makampuni yanahusiana na sekta ya afya.

Amesema kuwa kama chuo wanaungana na kushirikishana ujuzi ili kuweza kuendelea kukuza hadhi ya  chuo hicho.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo taaluma Profesa. Moshi Ntabaye amesema kuwa wanajivunia mafanikio wanayopata kila mwaka, na wapo mbioni katika ujenzi wa kampasi mpya ambayo itawasaidia kudahili wanafunzi wengi zaidi na ameiomba Serikali na wadau wa afya kuunga mkono jitihada hizo ili kuweza kuimarisha sekta ya afya nchini.
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza katika kongamano la kwanza la kitaaluma katika chuo kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki ambapo amewapongeza kwa kutoa mchango katika sekta ya afya na kuwataka kuongeza idadi ya wadahiliwa katika chuo hicho.
 Rais wa kongamano la kitaaluma chuo kikuu cha kumbukumbu ya Hurbet Kairuki Dkt. Leonard Malasa akizungumza na hadhara wakati wa kongamano hilo ambapo amesema kuwa wanashirikishana ujuzi na kushirikiana ili kuweza kukuza hadhi na thamani ya chuo hicho.
Naibu Makamu Mkuu (taaluma) wa chuo  kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki Dkt. Moshi Ntabaye  akizungumza wakati wa kongamano la kwanza la kitaaluma kufanyika chuoni hapo ambapo amesema kuwa wamejizatiti katika kuhakikisha wanashiriki vyema katika kuimarisha  sekta ya afya nchini.
 Katibu Mkuu Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akikabidhi zawadi kwa Michael Kalimba mmoja ya kati wanafunzi waliofanya vizuri kwa mwaka 2018, kulia ni makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa. Charles Mgone na kushoto ni Rais wa kongamano hilo Dkt. Leonard Malisa.(Picha na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad