HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 21 November 2018

IPP Automobile Ltd kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari ya Korea Kusini

KAMPUNI ya IPP Automobile Ltd imeingia ubia na Kampuni ya Youngsan ya Korea kusini kuwekeza katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi kwa kuwa na kiwanda cha kuunganisha magari nchini.
Gari la mwanzo kutoka katika uwekezaji huo wa zaidi bilioni 22, litaingia sokoni kati ya Septemba na Oktoba mwaka 2019.
Kiwanda hicho kinachotarajiwa kuunganisha magari 1000 kwa mwaka kitatoa ajira za moja kwa moja kwa wananchi 500, idadi inayotarajiwa kuongezeka kadri ya muda unavyokwenda.
Kiwanda hicho kitajengwa eneo la Kurasini, ujenzi utaanza mwanzoni mwa mwaka ujao.
Makubaliano ya uanzishwaji wa kiwanda hicho yalitiwa saini jijini Dar es Salaam jana kati ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi na Bw Thomas Choi Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea ambao ndio wawakilishi wa kiufundi wa kampuni ya Zyle Daewoo Commercial Vehicle na Hyundai Motor Corporation ya Korea Kusini huku tukio hilo likishuhudiwa na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Song Geum-young .
Katika mazungumzo wawakilishi hao na balozi walisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho, kumelenga kuunga mkono juhudi za maendeleo nchini.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti Mtendaji  wa IPP,Dk. Reginald Mengi alisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho, ilikuwa moja ya ndoto zake kama hatua ya kuitikia mwito wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, inayosisitiza kasi ya ujenzi wa viwanda nchini.
“Hakuna kinachoshindikana ukiwa na nia, hata Rais wetu anapambana katika mambo ambayo wengi waliona yanashindikana, amenunua ndege na  kufanya mengine mengi..hii ni hatua kubwa katika kukuza maendeleo yetu,” alisema Dk. Mengi.
Alisema kiwanda hicho kikianza kazi, kitatoa ajira kwa Watanzania, pia kitasaidia kuongeza mzunguko wa biashara katika Afrika Mashariki na Kati na kuiingizia mapato serikali kupitia kodi mbalimbali.
Aidha, alisema mipango yake ya baadaye ni kuhakikisha wanajenga kiwanda chenye uwezo wa kutengeneza magari kuanzia mwanzo hadi inapokamilika kutoka katika hatua hiyo ya uunganishaji, jambo alilosema litazidi kuitangaza Tanzania.
Magari yanayotarajiwa kuunganishwa kupitia kiwanda hicho ni mabasi, malori na magari madogo, ambapo kwa mujibu wa Balozi wa Jamhuri ya Korea, Mh. Song Geum-young magari hayo ni ya kisasa.
Alisema Jamhuri ya Korea imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa magari na kwamba anaamini kuwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho nchini, kutasaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya viwanda na kuleta tija kimaendeleo na amewahakikishia Watanzania kuwa Korea ni wajuzi wa kutengeneza magari yenye viwango vya juu vya ubora duniani.
Magari yatakayotoka katika kiwanda hicho ni ya biashara ya tani 2.5; 3.6 na malori  ya tani 18 hadi 28; mabasi ya mita saba,9 na 12 na magari ya kujinafasi  (SUV) na magari madogo mengine.
 Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi akizungumza katika hafla fupi ya kutiliana saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi kuunganisha magari hapa nchini iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea, Bw. Thomas Choi na kushoto Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mh. Song Geum-Young.
 Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mh. Song Geum-Young (kushoto) akizungumzia furaha yake kushuhudia utiaji saini huo unaounga mkono jitihada za kuigeuza Tanzania kuwa ya viwanda katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi na kulia ni Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea, Bw. Thomas Choi.
 Kutoka kushoto ni  Msaidizi wa Dk. Mengi, Bw. Godfrey Bitesigirwe, Mkurugenzi Mtendaji wa  IPP Touchmate, Bw. Victor Tesha pamoja na Mwandishi wa kampuni ya IPP Ltd, Bw. Abdulhamid Njovu wakishuhudia tukio hilo la utilianaji saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi kuunganisha magari hapa nchini katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi (kushoto) na Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea, Bw. Thomas Choi wakitiliana saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi kuunganisha magari hapa nchini katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kushoto waliosimama kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa  IPP Touchmate, Bw. Victor Tesha, Msaidizi wa Dk. Mengi, Bw. Godfrey Bitesigirwe pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mh. Song Geum-Young.
 Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi (kushoto) na Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea, Bw. Thomas Choi wakipeana mikono mara baada ya kutiliana saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi kuunganisha magari hapa nchini katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa  IPP Touchmate, Bw. Victor Tesha, Msaidizi wa Dk. Mengi, Bw. Godfrey Bitesigirwe pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mh. Song Geum-Young.
 Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mh. Song Geum-Young akimpongeza Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi mara baada ya tukio la utilianaji saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi kuunganisha magari hapa nchini katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mkurugenzi Mtendaji wa  IPP Touchmate, Bw. Victor Tesha (wa pili kushoto), Msaidizi wa Dk. Mengi, Bw. Godfrey Bitesigirwe (kulia) pamoja na Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea, Bw. Thomas Choi (nyuma ya balozi).
 Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi (kushoto), Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mh. Song Geum-Young (wa pili kulia), Msaidizi wa Dk. Mengi, Bw. Godfrey Bitesigirwe (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa  IPP Touchmate, Bw. Victor Tesha (wa pili kushoto) wakibadilishana mawazo mara baada ya ya tukio la utilianaji saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi kuunganisha magari hapa nchini katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi (katikati), Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mh. Song Geum-Young (wa pili kulia), Msaidizi wa Dk. Mengi, Bw. Godfrey Bitesigirwe (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa  IPP Touchmate, Bw. Victor Tesha (kushoto) pamoja na Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea, Bw. Thomas Choi (wa pili kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya ya tukio la utilianaji saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi kuunganisha magari hapa nchini katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za IPP jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad