HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 14 November 2018

GEREZA LUDEWA KUPATIWA TREKTA ILI KUONGEZA UZALISHAJI WA CHAKULA CHA WAFUNGWA

 Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike akisalimiana na Maofisa na askari wa Gereza Ludewa alipowasili kuendelea na ziara yake ya kikazi ya kutembelea magereza mbalimbali Mkoani Njombe, Novemba 13, 2018.
 Mkuu wa Gereza Ludewa, SSP. Akley Mkude(kushoto) akimweleza jambo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(kulia) alipotembelea gereza hilo  Novemba 13, 2018. Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo.
  Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike akipanda mti wa mparachichi katika Kambi ya Jeshi la Magereza ya Kidewa iliyopo Mkoani Njombe kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi Gereza Ludewa Novemba 13, 2018.
 Ghala la kuhifadhia mahindi yanayozalishwa katika Gereza Ludewa. 
 Baadhi ya Askari wa Gereza la Wilaya Ludewa  wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(hayupo pichani).
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Andrea Tsere(wa tatu toka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa tatu toka kulia) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani Ludewa( Picha na Jeshi la Magereza).

Na Lucas Mboje, Ludewa
KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike ameahidi kulipatia trekta moja Gereza la Kilimo Ludewa ili kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa.
Kamishna Jenerali Kasike ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na uongozi wa Gereza hilo baada ya kuwasili Wilayani Ludewa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa Jeshi hilo.
Amesema kuwa Gereza Ludewa ni miongoni mwa magereza 13 ambayo tayari yameainishwa katika mpango mkakati wa Jeshi la Magereza katika kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa waliopo magerezani hivyo lazima liwezeshwe zana za kilimo.
 “Nafahamu kuwa trekta lililopo hapa Gereza Ludewa ni la muda mrefu na ni chakavu, hivyo nitawapatieni trekta jipya ili muweze kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa”. Alisema Jenerali Kasike.
Pia, Kamishna Jenerali Kasike amehimiza uongozi wa Gereza hilo kuzingatia suala zima la uadilifu na amewataka kujiepushe na vitendo vyote vya ubadhilifu wa mali za umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza hilo, SSP. Akley Mkude amesema kuwa  katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2017/2018 gereza hilo lililima ekari 200 za mahindi na kufanikiwa kuvuna gunia zaidi ya 1700 ambazo zitatumika kulisha magereza yote ya Mkoa wa Njombe na Iringa. 
Aidha, ameongeza kuwa  malengo ya msimu huu wa mwaka 2018/2019 ni kulima ekari 700 za mahindi, ekari 40 za maharage, ekari 30 za alizaeti pamoja na bustani ekari 5 za mbogamboga. 
Gereza Ludewa lina eneo lenye ukubwa wa ekari 3500, Gereza hilo linajishughulisha na kilimo cha mahindi, maharage, alizeti pamoja na bustani za mbogamboga. Pia, linajishughulisha na miradi ya ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kuku wa kienyeji pamoja na uhifadhi wa mazingira.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad