HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 12, 2018

BENKI YA MAENDELEO TIB YATOA FEDHA KUSAIDIA UJENZI WA VITUO VYA MABASI MKURANGA NA KAHAMA

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
BENKI ya Maendeleo (TIB) imesaini mikataba ya msaada wa kiufundi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga  na Halmashauri ya Mji wa Kahama  na kwa mujibu wa mkataba huo benki ya TIB itatoa jumla ya shilingi 873,000,000 ili kusaidia Halmashauri hizo mbili kulipia gharama za wataalamu washauri watakaofanya upembuzi yakinifu na pia kuandaa michoro na makisio ya gharama na nyaraka za zabuni kwa ajili ya vituo vipya vya mabasi vitakavyojengwa kwenye Halmashauri hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa makubaliano hayo Kaimu Mkurugenzi uendeshaji wa Benki ya TIB Patrick Mongela amesema kuwa lengo la mkataba huo ni kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ina manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla, amesema kuwa wao kama Benki hawatoi mikopo pekee pia wanasimamia kikamilifu miradi ya kimaendeleo katika maendeleo ya jamii.

Amesema kuwa katika miradi hiyo Wilaya ya Mkuranga imepata jumla ya shilingi milioni 409.5 na kituo cha mabasi kitajengwa katika kijiji cha Kipala Mpakani na kituo hicho kitahudumia mabasi yaendayo Mikoa ya Kusini ikiwemo Lindi, Mtwara na Ruvuma na kwa upande wa Mji wa Kahama kituo cha mabasi kitakachojengwa kitarahisisha usafiri kwa wakazi wa Shinyanga, Singida, wakazi wa ukanda wa ziwa Victoria pamoja na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda.

Mongela amesema kuwa miradi itakayonufaika na mikataba hiyo  ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayopewa kipaumbele na Serikali ya awamu ya tano, na mradi utakaojengwa Wilayani Mkuranga ni moja ya miradi inayopangwa kutekelezwa na Serikali ili kuweza kusaidia kupunguza msongamano katika barabara za Dar es salaam.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filbeto Sanga ameishukuru benki ya TIB kwa msaada huo na amehaidi kuwa fedha hizo zitatumika ipasavyo katika kutekeleza mradi huo wa kimaendeleo.

Aidha Sanga amesema kuwa kituo cha mabasi ya kwenda Mikoa ya Kusini ilikuwa changamoto kubwa ila kwa ujenzi wa kituo hicho utarahisisha sana usafiri pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi na Serikali.

Pia Mkurugenzi wa Mji wa Kahama Anderson Msumba ameishukuru Benki ya TIB na  kusema kuwa Mji wa Kahama una wakazi wengi na mwingiliano ni watu mkubwa   na suala la stendi ni changamoto lakini kwa ujenzi wa mradi huo wakazi wa Kahama wawe tayari kupokea fursa hiyo katika biashara zao na pia mapato yatakayopatikana yatasaidia kuendeleza sekta nyingine za kimaendeleo zikiwemo afya na elimu.

Benki ya maendeleo ya TIB hadi sasa imetoa mikopo nafuu yenye ya thamani ya shilingi bilioni 7 ambayo imesaidia sana kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwemo viwanda, vituo vya mabasi, masoko na kanda maalumu za kiuchumi na miradi zaidi ya 40 imenufaika na mfuko huo ambao baadhi imekamilika na kupata wawekezaji kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, Serikali kuu, wadau wa maendeleo na wawekezaji binafsi.
 Kaimu Mkurungenzi wa Benki ya Maendeleo (TIB) Patrick Mongela akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utiaji wa saini za makubaliano baina ya Benki hiyo na Halmashauri za Mkuranga na Kahama katika utekelezaji ya mradi wa ujenzi wa vituo vya mabasi katika Halmashauri hizo.
 Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filbeto Sanga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuingia maakubaliano hayo na Benki ya maendeleo TIB ambapo Halmashauri hiyo imepata takribani shilingi milioni 490.2 ambazo zitatumika katika ujenzi wa kituo cha mabasi katika kijiji cha Mpala Mpakani Wilayani humo.
Mkurugenzi wa Manispaa  ya Kahama Anderson Msumba akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya makubaliano hayo ambapo jumla ya shilingi milioni 382.5 zilizotolewa na Benki ya maendeleo (TIB) zitatumika kujenga kituo cha basi katika mji wa Kahama. (Picha na Erick Picson, Blogu ya jamii)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad