HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 4, 2018

WALIMU TABORA WATAKIWA KUZINGATIA WARAKA WA ELIMU NAMBA 24 WA 2002 WAKATI WA KUTOA ADHABU YA VIBOKO

NA TIGANYA VINCENT
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu amewataka walimu katika shule mbalimabli mkoani humo kuzingatia Waraka wa Elimu namba 24  wa mwaka 2002 wakati utoaji adhabu za viboko kwa wanafunzi ili kuepuka kuingia katika matatizo na kushitakiwa kwa makosa mbalimbali.

Alisema lengo ni kuhakikisha wanapotoa adhabu za viboko kwa wanafunzi watukutuku wanazingatia matakwa ya Waraka huo na kuepuka kuingia tuhuma za kushitakiwa kwa makosa ya jinai kama yaliyotokea hivi karibuni mkoani Kagera.

Makungu ametoa kauli hiyo jana wakati wa kikao kazi cha siku moja na Maafisa Elimu Kata, Walimu wa wakuu wa shule za Msingi na Sekondari kutoka Wilaya ya Tabora, Wilaya ya Uyui na Sikonge ili kuwapitisha katika  mbalimbali zinazoongoza utendaji kazi wao.

Alisema kuna baadhi ya walimu wanasifika kwa utoaji wa adhabu ya viboko jambo ambalo ni hatari kwao na kwa ajira zao na familia zao.

 “Hivi walimu wenye tabia ya kupenda kuchapa viboko vingi kinyume cha maagizo ya waraka huu…wanafanya hivyo hivyo na kwa watoto wao au ni sawa na usemi usemao mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu”aliuliza.

Makungua alisema walimu wanadhamana kubwa ya kuwafundisha na kuwalea watoto kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi ili hatimaye waje kuwa viongozi na watumishi wema wa nchi hii.

Alisema Waraka huo unaeleza vizuri namna ya utoaji wa adhabu ya viboko izingatie ukubwa wa kosa, umri, jinsi, afya ya mtoto na visizidi vinne kwa wakati mmoja na kutaka mtoto wa kike adhibiwe na Mwalimu wa Kike labda kama hakuna.

Makungu aliongeza kuwa waraka huo unasema adhabu ya viboko itatolewa na Mwalimu Mkuu au mwalimu mwingine atakayeteuliwa na Makuu wa shule kwa maandishi lakini kuna baadhi ya walimu wamekuwa hawazingatii hilo ambalo ni kosa.

Aliwataka walimu hao kujitahidi kusoma nyaraka mbalimbali ambazo zinaongoza utendaji kazi wao ili kuepuka kuingia katika matatizo ambayo wanaweza kuyakwepa.

Naye Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Tabora (ELIMU) Susan Nussu alisema walimu wanapokuwa na watoto shuleni wanalojukumu la kufanyakazi ya kufundisha , kuwalea na kuwarekebisha watoto ambao ni watukutu.

Alisema sio vizuri kuwaacha watoto watukutu bila kuwarebisha kwa kufuata Sheria , Kanuni na taratibu ili nao warudi katika mstari na hatimaye waje wawe raia wema.

Nussu alisema kuwaacha au kuwakatia tamaa ni kujenga kundi la watumiaji wa  dawa za kulevya, majambazi na wahalifu wa siku za baadae. 
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu(katikati) akitoa ufafanuzi juu ya walimu kuzingatia  Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002 kuhusu adhabu ya viboko. Ametoa ufafanuzi huo jana wakati wa kikao kazi cha siku moja cha Maafisa Elimu Kata na Walimu wa Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kwa Wilaya za Tabora , Uyui na Sikonge. Wengine kwenye picha ni Katibu Tawala Msaidizi(ELIMU) Susan Nussu(kulia) na Afisa wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Tabora Shukuru Kazembe(kushoto)
Baadhi ya Maafisa Elimu Kata na  Walimu wa Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kutoka Wilaya za Tabora , Uyui na Sikonge wakiwa katika kikao kazi cha siku mjini Tabora jana kilichowaelimisha mambo mbalimbali ikiwemo uzingatiaji wa araka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002 kuhusu adhabu ya viboko

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad