HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 8 October 2018

SERIKALI HAITALIPA MADENI YALIYOKOPWA NA USHIRIKA-MAJALIWA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa zao la kahawa kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba, Oktoba 6, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya wadau wa zao la kahawa  wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba, Oktoba 6, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Awataka viongozi wa vyama vya ushirika wawe waaminifu

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka  viongozi wa vyama vya ushirika nchini kutumia vizuri rasimali za vyama hivyo na kwamba Serikali haitalipa deni lolote lililokopwa na vyama hivyo. 

“Biashara ya kununua madeni yaliyokopwa na vyama vya ushirika haipo kwenye Serikali hii ya awamu ya tano, badala yake itawachukulia hatua wote waliohusika na ubadhilifu huo.”

Pia Waziri Mkuu amepiga marufuku wafanyabiashara kuwaibia wakulima kwa kununua kahawa mbichi ikiwa shambani maarufu kama butura.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Oktoba 6, 2018) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wafanyabiashara pamoja na wadau wa zao la kahawa baada ya kuwasili mjini Bukoba kwa ajili ya ziara ya kikazi mkoani Kagera.

Waziri Mkuu amesema Serikali itachukua hatua kali kwa viongozi wa vyama vya ushirika ambao si waaminifu na wabadhilifu wa mali za ushirika.”Tunahitaji wakulima wapate fedha.”

Amesema Serikali itahakikisha wafanyabiashara wote, hususani wa mazao ya kilimo wanakuwa na mfumo sahihi wa ununuzi wa mazao utakao ongeza tija kwao na kwa wakulima.

Amesema kwa sasa Serikali inataka kuondoa mfumo uliopo wa vyama vya ushirika kufanya biashara na badala yake jukumu hilo libakie kwa wafanyabiashara.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara hao waihakikishie Serikali kwamba watanunua kahawa yote iliyopo kwa wakulima pamoja na kwenye vyama vya ushirika. Wafanyabiashara wameridhia kununua kahawa yote.

Awali, Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba alisema katika msimu wa mwaka huu jumla ya kilo 3,000,464 za kahawa isiyokobolewa  na kilo 8,191,86 za kahawa safi bado hazijanunuliwa.

Dkt. Tizeba alisema kahawa iliyobakia katika maghala ya vyama vya ushirika ni kama ifuatavyo, chama cha KCU (1990) kina kilo 1,1513 za kahawa isiyokoborewa na kilo 1,936, 367 za kahawa safi.

Pia chama cha KDCU kina kilo 6,012,840 za kahawa safi, Ngara Farmers C.S Ltd kina kilo 592,354 za kahawa isiyokobolewa na kilo 192,660 za kahawa safi.

“Nkwenda AMCOS ina kilo 175,553 za kahawa maganda na kilo 50,000 za kahawa safi na Magata AMCOS kina kilo 433,634 za kahawa safi.”

 Alisema vyama vya ushirika vinakabiliwa na changamoto ya kiwango kidogo cha kahawa kinachonunuliwa mnadani na wakati mwingine kutonunuliwa kabisa. Hali hii inatokana na kushuka kwa bei katika soko la dunia.

Alisema changamoto nyingine ni kuwepo kwa taarifa za upotoshaji kwa wakulima kutoka kwa walanguzi za kuzuia wakulima kukusanya kahawa yao kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi kwa wao  watanunua na kuwapatia bei nzuri.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad