HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 12 October 2018

Muhimbili waongeza siku saba kuhudumia Wananchi Musoma

Na John Stephen, Musoma
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeongeza siku saba zaidi kwa watalaam wake walioko Hospitali ya Rufaa Musoma ili kuhakikisha wanahudumia idadi ya wananchi wengi waliojitokeza kwa wingi kupata huduma katika kambi maalumu iliyoanza Oktoba 7, 2018 mkoani Mara.

Kambi hiyo ilitarajiwa kuisha leo Oktoba 12, 2018, lakini kutokana na hitaji kubwa la wananchi waliojitokeza kupata huduma, uongozi wa hospitali umeamua kuongeza siku hadi Ijumaa ijayo tarehe 19 Oktoba, 2018 ambapo watahitimisha na kurejea jijini Dar es  Salaam.

Hadi kufikia jana Alhamisi jumla ya wananchi  1210 walikuwa wamejiandikisha kupata huduma mbalimbali za matibabu kati hao   wananchi 1155 wameonwa na watalaamu  wa Muhimbili wale wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Musoma.

Kati ya hao, kinamama watano wamefanyiwa upasuaji, 36 wenye matatizo ya macho wamepatiwa huduma ya upasuaji, wagojwa wanane wamepatiwa huduma ya upasuaji wa mfumo wa mkojo, 14 upasuaji wa magonjwa mbalimbali (general surgery), 10 upasuaji wa masikio, koo na pua na  233 wamefaniwa uchunguzi wa kawaida.

Baadhi ya wagonjwa wamepewa rufaa za kwenda kutibiwa Muhimbili na wengine Hospitali ya Bugando ambako watafanyiwa uchunguzi zaidi na hatimaye kupata tiba stahiki kutokana na mazingira ya ugonjwa.

Hospitali ya Taifa Muhimbili ilipeleka watalaam wake 14 mkoani Mara katika Hospitali ya Rufaa ya Musoma mapema wiki hii ili kujenga uwezo wa watalaam na kutoa huduma kwa wananchi wenye matatizo mbalimbali  ya afya.

Philipo Jackson Mayunga mkazi wa Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ameomba uongozi wa Muhimbili kuongeza muda kwa wataalam wake kuendelea kutoka huduma kwa kuwa wametoka mbali kufuata huduma.

“Wataalam wamepewa muda mchache sana hivyo naomba waongezewe muda kwani watu wengi wanahitaji huduma za madaktari bingwa na wengine wamekata tamaa kwamba hawatatibiwa,” amesema Mayunga.

Kutokana na mahitaji ya wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Mara, Muhimbili imelazimika kuongeza muda kwa wataalamu wake ili kuhakikisha hakuna mtu yeyeyote atakayekosa huduma baada ya matibabu.
 Wataalam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakishirikiana na wataalam wa Hospitali ya Rufaa Musoma kufanya upasuaji kwa mgonjwa mwenye tatizo katika mfumo wa mkojo. Kutoka kulia ni mtaalamu wa chumba cha upasuaji, Anna Msafiri, Dkt. Isaack Mlatie, Dkt. Paul Masua na Dkt. Masanja.
 Dkt. Athuman Mbalamula wa Muhimbili akifanya upasuaji kwa mgonjwa mwenye tatizo sehemu ya tumbo kwa kushirikiana na mtaalamu wa upasuaji, Joram Laurent wa Hospitali ya Rufaa Musoma.
 Mmoja wa mgonjwa aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa Musoma akionwa na Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani wa Muhimbili, Dkt.  Brighton Mushengezi kwa kushirikiana na Mtaalam wa magonjwa ya ndani, Farbian Gabriel Beyesigwa  wa Hospitali ya Rufaa Musoma.
 Daktari bingwa wa macho wa Muhimbili, Dkt. Neema Kanyaro akitoa huduma ya macho kwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa macho leo katika Hospitali ya Rufaa Musoma.
 Mmoja wa watoto wenye tatizo kwenye koo akifanyiwa upasuaji leo na daktari bingwa Muhimbili, Dkt. Raymond Leiya.
 Wataalam wa upasuaji wa Hospitali ya Rufaa Musoma wakifanya upasuaji kwa kushirikiana na wataalam wa Muhimbili Dkt. Athuman Mbalamula na Dkt. Helen Mrina.
 Wataalam wa Muhimbili na wa Hospitali ya Rufaa Musoma wakifanya upasuaji wa macho jana katika Hospitali ya Mkoa wa Musoma.
Baadhi ya wagonjwa wakisubiri majibu katika maabara ya Hospitali ya Mkoa wa Musoma jana. Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad