HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 12, 2018

LEO KATIKA HISTORIA: NYERERE NA RAIA WAKAKAMAVU WA TANZANIA

Wakinamama Wako Mbele Katika Ulinzi wa Taifa

Na Judith Mhina-MAELEZO
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kiongozi aliyeshirikisha kila Mtanzania katika kujenga ukakamavu na kuwa sehemu ya ulinzi wa Taifa.
Hayo yamethibitika pale aliposhirikisha watoto, vijana, viongozi, wanaume kwa wanawake wa nyumbani, wenye kazi rasmi za serikali Taasisi, Mashirika ya Umma na binafsi katika Jeshi la kujenga Taifa, Jeshi la Mgambo na Chipukizi.
Akifunga mafunzo ya Mgambo kwa watumishi na wakazi wa Ikulu tarehe 1 Juni 1973,  kwa kikosi kilichoongozwa na Mama Maria Nyerere Mwalimu Nyerere  amesema “ Tanzania ina wajibu wa kujenga taifa kakamavu na imara kwa ajili ya ulinzi binafsi,  wa mipaka yetu,  Taifa na kujenga afya bora”
Mwalimu alithubutu kumshirikisha Mama wa Taifa ambaye ni Mke wake mwenyewe ili apate  mafunzo ya mgambo, kwa kujumuika na watumishi na wakazi wa Ikulu eneo ambalo waliishi yeye na familia yake.
Mwalimu ni kiongozi ambaye kwa mtazamo wa kawaida kila mmoja anaona anawajihi ambao haupatikani kwa watu wenye wadhifa kama wake kwa asilimia kubwa. Kitendo cha kumpeleka Mke wa Rais (mke wake mwenyewe) kujifunza mbinu za ukakamavu na ulinzi ni kiashiria tosha kwake kuwa watanzania wote ni sawa na anawapenda Watanzania kama anavyojipenda mwenyewe.
Hapa tunapata funzo ambalo Mwalimu Nyerere ametuthibitishia suala la kuwa mkakamavu ni la msingi hata ukiwa Mama wa nyumbani. Pia, ni sehemu ya kulinda afya yako ya mwili. Ukakamavu huo utakufanya kuwa mtu wa kufanya kazi na kuijifunza familia yako iwe sehemu ya mazoezi matokeo yake, ni familia yenye afya na kupunguzwa magonjwa yasiyoambukiza.
Akieleza chanzo cha Jeshi la Kujenga Taifa, Mkuu wa JKT Meja Generali Michael Isambuhyo akihojiwa na Televisheni ya ITV, amesema “Kabla ya Uhuru Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kiongozi wa Chama cha wafanyakazi, ambaye baadaye alikuja kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Rashid Mfaume Kawawa, walikuwa kwenye harakati za kuwaunganisha vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika harakati za Uhuru wa Tanganyika”.
Akiendelea kusimulia amesema kuwa kipindi hicho vijana walikuwa wamegawanywa na Wakoloni, mfano wasomi walifundishwa kuwa mabwana wakubwa, kwa ajili ya kuajiriwa katika kazi walizoziandaa wao. Wasio na elimu walidharauliwa na kuonekana wao ni daraja la chini la kuwatumikia wakubwa na kufanya kazi za uzalishaji mashambani.
Aidha, wengine walibaguliwa kwa misingi ya dini, eneo wanakotoka, kabila na rangi kwa kuona kuwa hawa ni bora kuliko wengine. Jambo hili lilifanyika Ili kudhoofisha harakati za kupigania uhuru. Mtazamo huu uIileta tatizo kubwa katika kuwaunganiisha na kuwaelimisha vijana kuwa wao ni wamoja,  wasikubali kubaguana kwa kuwa wana jukumu la kuleta uhuru wa Tanganyika. Amesema Mkuu huyo wa JKT.
Mwaka 1957, Mwalimu Nyerere akiwa kiongozi wa Tanganyika Afican National Union - TANU na Rashid Mfaume Kawawa akiwa kiongozi wa Shirikisho la wafanyakazi wa Tanganyika – TFL walialikwa katika sherehe za uhuru wa nchi ya Ghana.
Wakati wakiwa Ghana walipata bahati kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel wakati huo Bi Golden Meir na kupata fursa ya kubadilishana mawazo. Mwalimu alijua ukakamavu wa vijana wa Taifa hilo, hivyo akaomba kupewa fursa ya Israel kuwafunza vijana kutoka Tanganyika ombi ambalo lilikubaliwa. Alisema Mkuu wa JKT
Hivyo, kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa-JKT, kulitokana na mawazo ya Umoja wa Vijana wa Chama cha TANU (TANU Youth League), katika Mkutano wao Mkuu uliofanyika mjini Tabora tarehe 25 Aug 1962, chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Hayati Joseph Nyerere
Mkuu huyo wa JKT aliongeza kwa kusema kuwa “Mara baada ya uhuru, JKT lilianzishwa kwa sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (Nationa Service Act) ambayo ni sheria No 16 ya mwaka 1964. Sheria hii inatoa uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa kuandikisha vijana wa kulitumikia Jeshi hilo..

Jeshi la Kujenga Taifa limekuwa chimbuko la kuandaa vijana kuajiriwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini kama Jeshi la Wananchi wa Tanzania- JWTZ, Polisi, Magereza, Usalama wa Taifa na Taasisi binafsi za ulinzi. Hivyo Jeshi la Kujenga Taifa linachukua vijana wa kujitolea na mujibu wa sheria. Amesema Meja Generali Isumbuhyo.

Wakati wa uzinduzi wa JKT, Mwalimu Nyerere amesema “ Umuhimu wa JKT unatokana na Taifa kuhitaji huduma ya vijana na vijana kuitikia wito huo wa kulitumikia Taifa lao kwa jukumu lolote lihitajiwalo”.

Akielezea majukumu ya  Msingi ya  JKT, Mkuu huyo amesema kuwa suala la malazi au makazi , kupata mafunzo ya kufundishwa moyo wa kupendana bila kujali tofauti za itikadi, dini, kabila na kipato, Kupenda kazi za mikono., Kuthamini na kuendeleza mila, desturi na kudumisha utamaduni wa Taifa., Kuwa raia wema, wanaojiamini, wanaojituma, wenye uzalendo na kuipenda nchi yao.

Pili ulinzi wa Taifa, kwa , Kuwapa vijana mbinu za kijeshi wawe Jeshi la akiba, kuwaandaa vijana watakaofaa kujiunga na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.Kuwaandaa vijana kusaidia katika majanga mbalimbali, mfano mafuriko, moto na ajali mbalimbali.

Tatu, kazi ya uzalishaji mali,  Ili kuwafanya vijana wa kitanzania waepukane na kasumba kuwa kazi za ofisini ndio njia pekee na bora inayomuwezesha mtu kuishi, JKT linahusika na uzalishaji mali kwa lengo la kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta mbali mbali mara baada ya kumaliza mkataba na JKT.

Akifafanua uzalishaji mali huo unaofanywa na JKT ni pamoja na:,-Kujenga na kukarabati majengo, Viwanda na Kilimo, Madini na Nishati, Utalii, Ulinzi kwa Taasisi binafsi (Security Guard Services), Maduka (Super Market), Kuunganisha magari na mitambo na huduma za elimu JKT iliansishwa tarehe 10 Julai mwaka 1963 . Alimaliza Meja Generali Isambuhyo. 

Kwa kutambua umuhimu wa Taifa kakamavu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeliona suala hili la mazoezi kuwa ni muhimu. Yeye binafsi anafanya mazoezi, mfano hai Rais na Mke wake Mhe Mama Janeth Magufuli walipofanya mazoezi kutembea katia ufukwe wa feri na kupata fursa ya kusalimiana na majirani zao wa soko la Feri.
Kuhakikishia ulimwengu kuwa mazoezi ni muhimu katia  Taifa kakamavu la Tanzania, tarehe 16 Desemba 2016 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan alizindua Kampeni ya Kitaifa ya kuthibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza. 
Makamu wa Rais Mama Samia alishiriki kwa vitendo kufanya mazoezi ya viungo kwenye viwanja vya makazi yake Jijini Dar-es-salaam. Hii ikiwa ni sehemu ya kuendeleza kampeni ya Kitaifa ya kudhibiti magonjwa ya sio ya kuambukiza.  
Katika kuhakikisha Watanzania wanakuwa na utaratibu wa kujihusisha mna mazoezi ili kupunguzwa hatari ya kupata magonjwa ambayo sio ya kuambukiza, serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imesema kuwa, kampeni ya kuhamasisha   mazoezi ya “AFYA YAKO,  MTAJI WAKO, FANYA MAZOEZI, LINDA AFYA YAKO” itakuwa Endelevu na itafanyika nchi nzima.
Kampeni hiyo ilizinduliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki matembezi na kuzindua wa kampeni ya Kitaifa ya kudhibiti Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam.
Naye Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, amekuwa akisisitiza kufanya mazoezi ya mara kwa mara kwa Watanzania ili kuondoa magonjwa yasiyo ya lazima kutokana na jinsi jamii ya sasa inavyoishi haswa maeneo ya mijini.   
Alichosema Waziri Ummy ni sahihi kabisa hakuna sababu ya msingi ya serikali kupoteza fedha nyingi kununua madawa ya kutibu magonjwa ambayo kwa kufanya mazoezi tungeweza kuyazuia kama shinikizo la damu, kuumwa miguu kutokana na uzito uliopitiliza na magonjwa kama hayo.
Pia Waziri Ummy amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yanaongezeka sana duniani kote hasa kwenye nchi zilizoko chini ya Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania ambapo mpaka sasa yanachangia asilimia 27 ya vifo duniani.
Amesema utafiti uliofanyika mwaka 2012 ilihusisha Wilaya 53 hapa nchini imeonyesha viashiria hatarishi vya magonjwa ambapo asilimia 26 ya wananchi ni wanene kupita kiasi asilimia 26 wanalehemu nyingi mwilini na asilimia 25.9 wanashindikizo kubwa la damu.
Utafiti huo pia imeonyesha kuwa, asilimia 15.9 ya wananchi wanaovuta sigara na asilimia 97.2 ya wananchi wanakula mbogamboga na matunda chini ya mara tano kwa siku. Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema kuwa Watanzania wanaweza kukabiliana na magonjwa hayo kwa kufanya mazoezi ya viungo mara tatu kwa wiki kwa muda wa nusu saa. Aidha, ni muhimu kuchagua vyakula vinavyofaa na kupunguza matumizi ya pombe kupita kiasi na kujiepusha na matumizi ya tumbaku.  
 Rais Nyerere akikagua jeshi la mgambo kwenye sherehe ya kumaliza mafunzo yao Juni 01, 1973 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mwanamgambo Bibi Maria Nyerere akiwa tayari kuamrisha wanamgambo wenzake kwenye sherehe ya kumaliza mafunzo yao Juni 01, 1973 Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Wanamgambo wakipita mbele ya Rais Nyerere wakati wa sherehe ya kumaliza mafunzi ya mgambo Juni 01, 1973.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad