HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 31 October 2018

KUKANDA ASHUSHA RUNGU KWA WALIMU WATATU WA SHULE ZA MSINGI ZILIZOSHIKA NAFASI ZA MWISHO KITAIFA KUTOKA IGUNGA

Na TIGANYA VINCENT
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR TAMISEMI) Joseph Kakunda ameagiza kuvuliwa wadhifa wake Afisa Elimu Kata ya Malagano  Wilayani Igunga Raphael Kapela kwa kusema hawezi kuhamia kwenye kituo chake cha kazi kwa sababu ya kuwa na familia kubwa inayomtegemea.

Alisema kitendo cha Afisa huyo kuishi Nkinga badala ya Malagano kumesababisha Shule ya Msingi Malagano kufanya vibaya katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi ya darasa la saba mwaka huu.

Kakunda alichukua hatua hiyo jana wilayani Igunga wakati wa ziara yake ya kutembelea shule mbili za Shule ya Msingi zilizofanya vibaya na kisha kutembelea Shule ya Sekondari ya Bukoko ambayo Hosteli yake iliungua moto.

Alisema kuwa Afisa huyo kwa kitendo cha kusema kuwa hawezi kuishi Malagano kwa sababu hakuna nyumba za  kuishi watumishi na kwa sababu pia ana familia kubwa kinaonyesha kuwa hatoshi kushika nafasi hiyo.

Kakunda alisema kuwa nafasi hiyo ichukuliwe na mtu mwingine ambaye atakuwa tayari kuishi Malagano hata kama ni nyumba ya nyasi ili aweze kusimamia maendeleo ya elimu na nidhamu ya walimu katika Shule hiyo ili isifanye vibaya tena.

Alisema kitendo cha Mtumishi kukaa sehemu kwa sababu ya kuwepo kwa nyumba ya nyasi hakiwezi kuwa kinga na uhalali kwake kuishi mbali na kituo chake cha kazi kwa sababu kinapunguza ufanisi katika kutekeleza majukumu yake.

 “Waziri Mkuu alishatoa agizo watumishi wote wa umma kuishi karibu vituo vyao yao vya kazi…kitendo cha baadhi ya watumishi kuishi nje ya vituo vyao ni kudharau agizo la Waziri Mkuu na kukiuka taratibu za utumishi wa umma…kuanzia sasa ni marufuku kwa mtumishi kuishi nje ya kituo chake cha kazi …naagiza Mamlaka za Nidhamu ziwachukulie hatua watumishi ambao bado wanaendelea kuishi  nje ya vituo vyao vya kazi” alisema.

Wakati huo huo Naibu Waziri huyo ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Igunga kuwachukulia hatua Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwazizi na Afisa Elimu Kata ya Bukoko kwa makosa mbalimbali ikiwemo kushindwa kusimamia nidhamu ya walimu wao.

Alisema Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Musa Kitenya amekiri kukosa uzoefu kwa nafasi hiyo na hivyo kushindwa kuwasimamia Walimu waliochini yake na kusababisha utoro na wengine kuchelewa kazini miongoni na hivyo kuifanya shule hiyo kuwa ya pili kutoka mwisho nchini baada ya kufaulisha mwanafunzi mmoja kati ya wanafunzi 42.

Alisema Mwalimu Mkuu alikiri kuteuliwa mwaka huu Mwezi Machi na hivyo hana uzoefu wa kusimamia walimu wenzie kwa kuwa bado ni mgeni katika Cheo hicho.

Kakunda alipendekeza Mwalimu ashushe cheo na asihamishe ili aendelee kufundisha katika Shule hiyo chini usimamizi wa Mwalimu Mkuu mwingine.

Kwa upande wa makosa yanayomkabili Afisa Elimu Kata  ya Bukoko Simon Masele , Naibu Waziri alisema ni pamoja na kushindwa kuwasimamia walimu wa Shule hiyo na kuwafanya wawe watoro na wengine wachelewe kufika kazi na kufanya ufundishaji kuwa duni na usioridhisha.

Alisema kosa jingine ni kushindwa kutoka taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga juu ya tatizo la nidhamu miongoni mwa walimu wa Shule ya Mwazizi na kuwafanya waeneleo , hali iliyofanya wanafunzi wafeli vibaya.

“Kwa kweli lazima niseme nyie Walimu na Afisa Elimu Kata wenu hakuwatendea haki wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi na wale ambao bado wanaendelea na masomo kwa sababu ya nidhamu mbovu inayoambatana na utoro na uchelewaji miongoni mwenu na kufanya watoto wasifundishwe vipindi vyote kwa mujibu wa matakwa ya mihitasari” alisema

“ Afisa Elimu Kata unadai uliwaandikia barua …Utandikaje barua ya kuwataka kujieleza bila kupeleka nakala kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri…nikisema barua hizo ziliandikwa kirafiki na kwa lengo la kurindana nitakosea?…kwa nini usimpe nakala Mkurugenzi ili aone kuwa umejaribu kuchukua hatua …unaona tatizo unakaa kimya …hilo halikubaliki” alisema.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ameuagiza uongozi wa Halmshauri ya Wilaya ya Igunga kuwa hakuna kuwahamisha walimu kutoka Shule ya Mwazizi , badala yake wanatakiwa kuwa katika uangilizi wa mwaka mmoja wa utendaji kazi wao ili kuona kama wamebadilika na kama  wanaendelea na tabia hiyo wachukuliwe hatua kulingana na taratibu za ajira zao.

Aidha Naibu Waziri alisema kuwa wa mwisho sio tatizo bali tatizo ni ufaulu mbaya kwani hata wote wangepata alama A lazima angekuwepo wa mwisho kinachosistizwa ni kuhakikisha watoto wanafanya vizuri.

Shule ya Mwazizi imeshika nafasi ya 448 kati ya shule 448 mkoani Tabora na imekuwa ya 10,0089 kati ya 10,0090 nchini baada ya watoto 42 kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na kufaulisha mtoto mmoja.

Wakati shule nyingine ya Malagano imeshika nafasi 447 kati ya shule 448 mkoani Tabora na 10,0087 kati ya 10,0090 nchini.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Joseph Kakunda akiongeza jana na baadhi ya Viongozi na wanakijiji  alipotembelea Shule ya Msingi Mwazizi kufuatilia kwanini ilifanya shule hiyo ilifanya vibaya katika mtihani wa kumaliza la saba na kuwa ya pili kutoka mwisho kitaifa.
 Mwalimi Mkuu wa Shule ya Msingi Mwazizi wilayani Igunga Musa Kitenya akisoma taarifa jana inayoonyesha sababu za kufanya vibaya kwa shule yake katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na kuifanya kuwa ya pili kutoka mwisho kitaifa.
 Baadhi ya Viongozi na wanakijiji wa Kijiji cha Mwazizi wakimsikiliza jana Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (hauyopo kwenye picha) wakati alipotembelea Shule ya Msingi Malagano kufuatilia kwanini ilifanya shule hiyo ilifanya vibaya katika mtihani wa kumaliza la saba na kuwa ya pili  kutoka mwisho kitaifa.
 Wanafunzi wa Shule ya Msingi Malagano wakiwa mapunziko jana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad