HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 2, 2018

BENKI YA KILIMO YAOMBWA KUSAIDIA ZAO LA CHAI WILAYANI LUSHOTO

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeombwa kusaidia uzalishaji wa zao la chai wilayani Lushoto mkoani Tanga ili kuchagiza shughuli za kiuchumi na kunyanyua kipato cha wakulima wadogo wadogo wilayani humo humo.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. January Lugangika wakati akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine alipotembelea Ofisini kwake.

Bw. Lugangika alisema kuwa Serikali imejipambanua katika kukufua viwanda hasa vyenye kusaidia wakulima wadogo wadogo kupitia ununuzi wa malighafi akilitaja zao la chai kuwa ni la kipaumbele katika kuchagiza juhudi hizo za Serikali.

“Benki ya Kilimo ikisaidia kufufua viwanda vyetu vya chai itawanufaisha wakulima wetu wanaolima chai hivyo kuweza kunyanyua kipato cha wakulima wilayani kwetu,” alisema.

Aliongeza kuwa wilaya ya Lushoto imejaliwa kuwa na eneo kubwa la uzalishaji zao la chai hivyo kuongeza tija katika kuendeleza zao hilo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine alisema TADB ipo tayari kuchagiza uzalishaji wa mazao ya kimkakati yenye masoko ya uhakika ikiwemo zao la chai na yenye kulenga kunyanyua hali za maisha ya wakulima wadogo wadogo nchini.

Aliongeza kuwa TADB ipo tayari kusaidia juhudi za wilaya ya Lushoto katika kuwasaidi wakulima walio kwenye vikundi vya ushirika au skimu za uzalishaji wa mazao ya kilimo wilayani humo.

"TADB ipo tayari kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini,” alisema.

Bw. Justine aliongeza kuwa Benki  ya Kilimo imelenga kutekeleza kwa vitendo Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP 2) kwa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo nchini kwa kuwapatia mikopo ya gharama nafuu ili kuongeza uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda hivyo kuchagiza dhana ya Tanzania ya Viwanda.

Naye, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bw. Nicodemas Tambo aliiomba Benki ya Kilimo kuwaelimisha wakulima wa wilaya hiyo juu ya uwepo fursa za mikopo ya gharama nafuu kutoka TADB.

“Nawaomba muwaelimishe wakulima wetu ili wachangamkie fursa za huduma zenu ili waweze kulima kibiashara,” alisema.
 Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Bw. January Lugangika (wapili kushoto) akizungumza na ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ulipomtembelea Ofisini kwake wilayani Lushoto kkuzungumzia fursa za uwekezaji katika kilimo. Wanaomsikiliza ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine (kushoto), wengine ni Afisa Biashara Mwandamizi wa TADB, Eunice Mbando (kulia) na Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo, Bw. Tito Kayugyuma (wapili kulia).
 Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Bw. January Lugangika akihimiza jambo wakati wa kikao.

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine akifafanua jambo wakati akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Bw. January Lugangika (hayupo pichani).
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine (kulia) akiwa katika mazungumzo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Lushoto, Bw. Nicodemas Tambo (katikati). Anayesikiliza ni Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo, Bw. Tito Kayugyuma (kushoto).
 Katibu Tawala wa Wilaya ya Lushoto, Bw. Nicodemas Tambo akizungumza wakati wa kikao hicho alitumia fursa hiyo kuiiomba Benki ya Kilimo kuwaelimisha wakulima wa wilaya hiyo juu ya uwepo fursa za mikopo ya gharama nafuu kutoka TADB.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Lushoto, Bw. Nicodemas Tambo (kushoto) akiagana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine (kulia) mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad