HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 17, 2018

WABUNGE WA MAJIMBO YALIMAYO KAHAWA WAUNGA MKONO JUHUDI ZA DKT TIZEBA KWA KUIMARISHA USHIRIKA

Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akizungumza mara baada ya Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo kutoa ufafanuzi kuhusu zao la kahawa wakati akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini, Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma.
Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo akitoa ufafanuzi kuhusu zao la kahawa wakati akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini kwa Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi mkutano uliohudhuriwa na wabunge kutoka maeneo yote yanayozalisha kahawa, Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma.

Wabunge wa maeneo yote yanayozalisha kahawa nchini wakifatilia taarifa iliyowasilishwa na Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo mbele ya Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Tarehe 14 Septemba 2018 kwenye ukumbi wa White House Mjini Dodoma.

Na Mathias Canal-WK, Dodoma
Ushirika ni dhana ya kuleta maendeleo kwa kushirikiana, Dhana hii imetajwa kuwa imefanikiwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, Kutokana na changamoto mbalimbali zilizoikumba sekta hii ya ushirika watu wengi walikosa imani na vyama hivyo kutokana na viongozi wake kutokuwa waaminifu (Wabadhilifu).

Hayo yalibainishwa juzi tarehe 14 Septemba 2018 na wabunge kutoka maeneo yote yanayozalisha kahawa nchini hususani katika mikoa ya Kagera, Mara, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, na Manyara wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini kwa Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa mikutano wa CCM Makao makuu maarufu kama White House

“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili hivi tangu Mhandisi Mhe Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo wakati kushika nafasi katika wizara hii amefanya kazi kubwa mno, imani kwa vyama vya ushirika imeongezeka na vyama vingi vinaendelea kuundwa hasa vile vya kuweka na kukopa, yaani SACCOS” Walisema

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Makongoro Nyerere, Naibu waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba, wataalamu kutoka wizara ya kilimo akiwemo Naibu katibu Mkuu Prof Sizya Tumbo, Mrajis wa vyama vya ushirika,vyama vya ushirika na wawakilishi wa wakulima kutoka maeneo yanayolima kahawa.

Wabunge hao walitaja kuwa ushirika ni sekta mtambuka inayohusisha sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Madini, Viwanda, Nyumba na Fedha (Ushirika wa Akiba, Mikopo na Benki) ambazo zinagusa wananchi wengi zaidi hivyo kutokana na maelezo ya kuridhisha yaliyotolewa na Dkt Tizeba katika taarifa yake ya mwenendo wa zao la kahawa ni wazi kuwa yameridhiwa hivyo wabunge hao wameunga mkono na kuihubiri dhana ya ushirika kwa asilimia 100%.

Katika taarifa hiyo Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba alisisitiza kuwa kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Wizara kupitia Tume ya maendeleo ya ushirika imeendelea kuwezesha na kuimarisha ushirika ili wananchi waweze kunufaika na fursa zinazopatikana katika ushirika kwa lengo la kuchangia katika kuongeza kipato kwa wananchi wengi hususani waliopo vijijini.

Alisema katika mwaka 2017/2018, Tume imefanya uhamasishaji wa wananchi kujiunga au kuanzisha vyama vya ushirika ambapo hadi kufikia Disemba 2017 vyama vipya 394 vilisajiliwa na kufanya idadi ya vyama vya ushirika kufikia 10,990 kutoka 10,596 vilivyokuwepo Machi 2017.

Alisema vyama hivyo vinakadiriwa kutoa ajira mpya kwa wananchi takribani 1,182 huku katika kipindi cha mwaka 2017/2018 wanachama wapya 385,295 walijiunga au kuanzisha vyama vya ushirika na kufanya idadi ya wanachama kuongezeka kutoka 2,234,016 hadi kufikia 2,619,311

Alisema kuwa uanzishwaji wa vyama vingi vya ushirika kwa sasa unatokana na elimu watu wengi waliyoipata kuhusu Ushirika na watu kuendelea kuelewa kuwa changamoto zilizoko ndani ya ushirika zinatatulika ikiwa ni pamoja na hivi karibuni kutangaza kiama kwa baadhi ya viongozi wabadhilifu wa vyama hivyo ambao wanautumia ushirika kama sehemu ya kujinufaisha wao pasina kuwa na mtazamo wa mafanikio kwa wanachama wote.

Alisema, Dhamira ya Ushirika ni nzuri na kama itafanya kazi vizuri ni njia nzuri ya kuleta mabadiliko kwa watu wengi huku akisisitiza Wanachama wa Ushirika kujiimarisha katika misingi ya uaminifu, uwazi, uwajibikaji kwa jamii na kuwajali wengine.

Dkt Tizeba alisema Ushirika ni muungano wa watu ambao wanafanya kazi pamoja kwa hiari ili kufanikisha mahitaji yao ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kupitia shughuli ya biashara inayomilikiwa kwa pamoja na kudhibitiwa kidemokrasia kwani njia pekee yenye tija na mafanikio ya kilimo kwa mkulima ni kuuza mazao yao kupitia mfumo huo rasmi wa ushirika.


“Kupitia ushirika kutamfanya mkulima kujihami na bei kwa kuuza kwa pamoja kwani kwa muda mrefu kilimo cha masoko kimekuwa kikitengenezwa na wakulima wenyewekwa sababu ya kutojiunga pamoja na kuwa na mfumo rasmi” Alikaririwa Dkt tizeba na kuongeza kuwa


“Kunapokuwa na chama imara cha Msingi, chama hiki kinaunda chama kikuu kilicho imara kwa kufanya hivyo tutaondokana na uduni wa bei kwa mkulima kutokana na kushuka bei kwa mazao kwa sababu ya mkulima mmoja mmoja kuuza mazao yake mwenyewe” Alisema


Waziri huyo wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba alisema Serikali imeamua kufufua ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima. "Tumeamua kurudisha ushirika aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo kwa viongozi waliopata dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda kupata ulaji.” Alisema


Kwa upande wake Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akizungumza mara baada ya mjadala huo kutuama kwa masaa 8 kujadili namna ya kupata masoko ya mazao ya kilimo, urahisi wa upatikanaji wa mitaji, siasa ya kilimo kupitia ushirika na maandalizi ya miundombinu rafiki katika kilimo, alisema katika kipindi cha miaka mitano Chama Cha Mapinduzi kupitia ilani ya ushindi ya mwaka 2015-2020 kimeweka kipaumbele cha kuhakikisha kuwa kilimo nchini kinakuwa endelevu na chenye tija ili kuliwezesha Taifa kuwa na utoshelevu wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima na kuwa chanzo cha kuaminika cha malighafi ya sekta ya viwanda.


Dkt Bashiru alinukuu ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 katika sura ya pili ibara ya 22 inayosisitiza kuviimarisha na kuviwezesha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa za masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji wa thamani na biashara.


Aidha, Dkt Bashiru alisimsisitiza Mrajis wa Vyama vya ushirika nchini kuongeza ufanisi katika kuwajengea uwezo viongozi wote wa Vyama vya ushirika ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad