HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 7, 2018

VYUO VIKUU VIWE NA BODI ILI KULINDA MASLAHI YA WANAFUNZI NA WAHADHIRI

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii

MBUNGE wa Manonga Mh. Seif Gulamali amependekeza kuwepo kwa bodi maalumu itakayowaongoza wahadhiri wa vyuo vikuu kiutendaji na kinidhamu.

Akichangia katika mjadala wa kupitisha muswada wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  kuhusiana na uanzishwaji wa bodi ya kitaalamu ya walimu nchini ambayo itakuwa na majukumu ya kuinua viwango vya utaalamu wa Ualimu kwa lengo la kuhakikisha walimu wanakuwa na viwango stahiki kitaaluma na kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya ualimu.

Gulamali ameunga mkono muswada huo na kuongeza kuwa isiwe kwa walimu pekee bali ilenge kwa wahadhiri pia ambao  wana wana umoja wao kama UDOMASA kwa wahadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma na UDASA kwa chuo kikuu cha Dar es saalam.

Ameeleza kuwa vyuo vyenye umoja huo lazima kuwe na bodi moja ambayo itawaongoza na majukumu ya bodi iwe ni pamoja na kusajili wataalamu hao kwa ngazi za shahada, uzamili na uzamivu na kujua idadi yao ili kuweza kuwa na takwimu sahihi za idadi ya wataalamu hao.

Pia ameshauri kuwa bodi hiyo iwe na kazi ya kutambua uwezo wao kitaalama sambamba na kusimamia nidhamu hasa malalamiko ya wanafunzi hasa wakike juu ya wahadhiri kwa manyanyaso ya kijinsia.

Aidha amesema kuwa bodi hizo zitakuwa na maslahi kwa pande zote mbili  wawezeshaji na wawezeshwaji katika elimu ili kuweza kuzalisha wataalamu wengi na bora zaidi.

Muswada huo uliopita Bungeni utawalenga walimu katika ngazi zote waliohitimu katika vyuo vinavyotambulika kwa ngazi ya Shahada, stashahada na astashahada na utashirikisha taasisi na wizara mbalimbali zikiwemo Utumishi wa Umma, Chama cha Walimu, Maafisa elimu, Wizara ya mambo ya ndani na Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad