HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 17 September 2018

TRA YATOA ELIMU YA MAADILI, MABADILIKO YA SHERIA ZA KODI KWA WATUMISHI WAKE TANGA

Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Tanga Masawa Masatu akizungumza wakati wa utoaji elimu ya Maadili na Mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa watumishi TRA mkoani hapo kwa lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza na kusimamia sheria za kodi kwa ufanisi na kutoa huduma stahiki kwa wateja.

Na Veronica Kazimoto, Tanga

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu ya maadili na mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa watumishi wake mkoani Tanga kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waweze kutekeleza na kusimamia sheria za kodi kwa ufanisi na kufuata maadili ya kazi ipasavyo.

Akizungumza wakati akiwasilisha mada ya Mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Mwaka 2018, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla kutoka TRA Makao Makuu amesema kuwa, kila mtumishi wa TRA anapaswa kujua sheria za kodi na mabadiliko yake kwa undani ili aweze kutoa huduma stahiki kwa wateja.

"Kila mwaka wa fedha unapoingia, Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hufanya mabadiliko mbalimbali ya sheria na kanuni za ukusanyaji wa kodi, hivyo ni muhimu kila mtumishi wa TRA kujua mabadiliko na kanuni hizo kwa lengo la kutoa huduma stahiki kwa wateja wetu,"  alisema Masalla.

Aidha, Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amewataka watumishi hao kufuata sheria na kuepuka upendeleo wakati wote wanapotoa huduma kwa wateja wanaotembelea ofisi za TRA.

Naye, Afisa Maadili Mwandamizi Adelaida Rweikiza kutoka TRA Makao Makuu, amewaambia watumishi hao kuwa, ni muhimu kuzingatia maadili kila wanapotimiza wajibu wao ili kuondoa malalamiko ambayo yanaharibu taswira nzuri ya TRA.

"Kila mmoja wetu ana jukumu la kuilinda taswira ya mamlaka yetu, hivyo ni wajibu wetu kuzingatia maadili ikiwa ni pamoja na kutumia lugha nzuri kila tunapowahudumia wateja," alisema Rweikiza.

Timu ya Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kutoa elimu ya maadili na mabadiliko ya Sheria za Kodi ikiwa ni pamoja na Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya Kodi kwa watumishi wa TRA na wafanyabiashara wa Mikoa ya Kanda ya Kasikazini.
Afisa Maadili Mwandamizi Adelaida Rweikiza kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu akizungumza na watumishi wa TRA mkoani Tanga wakati wa utoaji elimu ya Maadili na Mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa watumishi hao kwa lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza na kusimamia sheria za kodi kwa ufanisi na kutoa huduma stahiki kwa wateja.
Afisa Kodi Mwandamizi Gelas Kinabo wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Tanga akichangia hoja wakati wa utoaji elimu ya Maadili na Mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa watumishi TRA mkoani hapo kwa lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza na kusimamia sheria za kodi kwa ufanisi na kutoa huduma stahiki kwa wateja. 
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu akiwasilisha mada kuhusu mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa watumishi wa TRA mkoani Tanga kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waweze kutekeleza na kusimamia sheria za kodi kwa ufanisi na kutoa huduma stahiki kwa wateja.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad