HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 21 September 2018

TRA YAENDELEA KUWAPIGA MSASA WATUMISHI WAKE

Na Veronica Kazimoto
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kutoa elimu ya maadili na namna bora ya kuhudumia wateja kwa watumishi wake nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao na kuwaongezea weledi katika majukumu yao ya kila siku.

Akiwasilisha mada kuhusu Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma kwa Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika ofisi ya TRA Moshi mkoani Kilimanjaro, Afisa Maadili Mwandamizi wa mamlaka hiyo Adelaida Rweikiza amesema kuwa  ni wajibu wa watumishi wote wa TRA kuwahudumia wateja kwa usawa na kwa kiwango cha hali ya juu.

"Ni wajibu wetu sisi watumishi wa TRA kuhakikisha tunatoa huduma bora pamoja na kutumia lugha nzuri kila tunapowahudumia wateja wetu," alisema Rwikiza.

Rweikiza ameongeza kuwa, maadili katika Utumishi wa Umma  ni jambo la msingi hivyo amewasisitiza watumishi hao kuwa waadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa na mienendo mibaya ambayo inaweza kuharibu taswira ya TRA.

Naye, mmoja wa watumishi hao ambaye ni Afisa wa Kodi Robert Mlay amefurahishwa na kitendo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoa elimu kwa watumishi wake na kufafanua kuwa, elimu hiyo itawasaidia katika kuongeza ufanisi na kutimiza malengo ya mamlaka.

"Nimejisikia vizuri sana kupata elimu hii ya maadili na namna bora ya kuwahudumia wateja kwasababu itatusaidia sisi kama watumishi wa TRA kutoa huduma kwa haki bila upendeleo wowote," alieleza Mlay.

Kwa upande wake Afisa Kodi Mwandamizi ambaye pia ni mtumishi aliyepata elimu hiyo Gloria Ngowi, ameeleza kuwa ni muhimu elimu ya maadili ifundishwe kwenye vyuo vyote ili vijana wanapoajiriwa katika taasisi mbalimbali waweze kufanya kazi zao kwa kufuata misingi ya maadili.

"Ninaiomba mamlaka iendelee kutoa elimu hii kwa ajili ya kutukumbusha wajibu wetu mahali pa kazi lakini pia kuna umuhimu wa vyuo vyetu nchini kufundisha somo la maadili kwa lengo la kuwawezesha vijana wetu kufuata misingi ya maadili kila wanapotimiza majukumu yao", alifafanua Ngowi.

Elimu ya Maadili na namna bora ya kuhudumia wateja inaendelea kutolewa kwa watumishi mbalimbali wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakati elimu ya Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye Malimbikizo ya Madeni ya Kodi na Mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 ikitolewa kwa wafanyabiashara.
 Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro Msafiri Mbibo akizungumza wakati wa utoaji elimu kwa wafanyakazi wa TRA Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro  iliyofanyika leo kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waendelee kutoa huduma bora na stahiki kwa wateja wao.
  Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Adelaida Rweikiza akiwasilisha mada kuhusu Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma wakati wa utoaji elimu kwa wafanyakazi wa TRA Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro  iliyofanyika leo kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waendelee kutoa huduma bora na stahiki kwa wateja wao.
  Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Diana Masalla akijadiliana jambo na Afisa Kodi Mwandamizi wa mamlaka hiyo Shaban Makumlo wakati wa utoaji elimu kwa wafanyakazi wa TRA Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro  iliyofanyika leo kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waendelee kutoa huduma bora na stahiki kwa wateja wao.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakisikiliza kwa makini mada kuhusu Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma wakati wa utoaji elimu kwa wafanyakazi hao iliyofanyika leo kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waendelee kutoa huduma bora na stahiki kwa wateja wao. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad