HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 7 September 2018

PPRA yawapa wahandisi ufafanuzi fursa ya ununuzi kwa njia ya mtandao

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imeendelea kuwapa wadau wake elimu na ufafanuzi kuhusu fursa na faida za kutumia mfumo wa ununuzi wa njia ya mtandao (TANePS).
Mamlaka hiyo imetumia fursa ya maonesho ya mkutano wa 16 wa mwaka wa Wahandisi yaliyoandaliwa na Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), yaliyofanyika Septemba 5 hadi 7 jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, PPRA ilikuwa inapokea maoni na kujibu maswali mbalimbali yaliyohusu mfumo wa ununzi kwa njia ya mtandao (TANePS) pamoja na masuala yanayohusu marekebisho ya sheria ya manunuzi ya umma yaliyofanyika mwaka 2016.
Katika maboresho ya sheria ya ununuzi wa umma, wahandisi walijikita zaidi katika marekebisho ya kanununi Na. 55A, 55B, 55C NA 55D, kama walivyoelezwa na mgeni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kuwa kupitia maboresho ya sheria ni vyema wakachangamkia fursa za miradi ya serikali kuliko kulalamika kila wakati kuwa wanakosa miradi hiyo na kupewa kampuni za nje ya nchi.
Akizungumziaa kuhusu mfumo wa ununuzi wa umma (TANePS), Mhandisi Mwanahamisi Ally wa kampuni ya Classic Plan alisema kuwa baada ya kujiunga na TANePS anaona mwanga wa kupungua kwa mianya ya rushwa na urasimu katika michakato ya manunuzi ya umma, hivyo akawaomba PPRA waendelee kutoa elimu zaidi kwa wahandisi na wazabuni kwa ujumla ili wasipitwe na fursa hiyo muhimu.
“Leo nimepata ufafanuzi zaidi zaidi kuhusu maeneo ambayo nilikuwa na maswali  zaidi baada ya kujisajili na kupata mafunzo ya kuutumia mfumo huu wiki kadhaa zilizopita,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kupata ufafanuzi, alitaka kufahamu ni lini fursa za zabuni zitaanza kutangazwa kwa njia hiyo ili aanze ‘kuchangamkia’ fursa hiyo muhimu isiyo na urasimu na inayohuisha uwazi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu swali hilo, Afisa Tehama wa PPRA, Giftness David alisema kuwa kwa sasa baadhi ya taasisi zimeshawasilisha mpango wa manunuzi kwa njia ya TANePS, na kwamba kwa ujumla takribani wazabuni 1000 wamekwisha jiandikisha kwenye mfumo huo, hali inayoashiria utayari zaidi.
Aidha, Mhandisi Tumaini Msaki aliungana na idadi nyingine ya wahandisi kuuliza maswali ya sheria ya manunuzi ya umma, hususan kuhusu marekebisho ya sheria na kanuni ya mwaka 2016.
“Mimi nilitaka kufahamu ni kwa kiasi gani wahandisi wa ndani wanapewa nafasi ya kufanya kazi na Serikali kupitia zabuni mbalimbali ambazo makampuni ya nje yanakuwa yanashindania pia kwa kuwa wenzetu wana nguvu zaidi ya kifedha na mitambo,” alisema Mhandisi.
Aliongeza kuwa alijibiwa na kuoneshwa jinsi ambavyo sheria inatoa nafasi ya upendeleo kwa wazabuni wa ndani wanapokuwa wanashiriki zabuni zinazohusisha makampuni ya nje pia. Alisema kuwa sheria hiyo inatoa hadi upendeleo wa asilimia 10 kwa wazabuni wa ndani katika hali hiyo.
TANePS, ni mfumo wa manunuzi kwa njia ya mtandao unaoratibiwa na PPRA kwa kushirikiana na taasisi za Serikali ambao ni wadau wa manunuzi. Mfumo huu ulizinduliwa rasmi Juni mwaka huu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. 
 Afisa Tehama wa PPRA, Giftness David, akijibu maswali ya wahandisi kuhusu TANePS katika maonesho ya mkutano wa 16 wa mwaka wa Wahandisi yaliyoandaliwa na Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), yaliyofanyika Septemba 5 hadi 7 jijini Dar es Salaam.
Afisa Uhusiano wa PPRA, Nelson Kessy, na Afisa Tehama, Siganike Baruti wakitoa ufafanuzi kwa wazabuni kutoka kampuni ya Bizcyclone katika maonesho ya mkutano wa 16 wa mwaka wa Wahandisi yaliyoandaliwa na Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), yaliyofanyika Septemba 5 hadi 7 jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad