HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 9 September 2018

MKUU WA WILAYA YA TEMEKE AUNGANA NA BENKI YA KCB KUFANYA USAFI MBAGALA ZAKHEM

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
 Mkuu wa Wilaya ya Temeke  Mh. Felix Lyaniva akishirikiana na wafanyakazi wa Benki wa KCB pamoja na   wafanyabiashara wa eneo la Mbagala Zakhiem wamefanya  usafi kwa pamoja katika eneo hilo ikiwa ni kuweka mazingira safi na salama.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mh. Felix Lyaniva ameiomba Benki ya KCB  kutoa huduma nzuri na bora kwa wakazi wa Mbagala, na ikiwezekana kuwapa punguzo la riba na masharti nafuu katika mikopo ili kuweza kupata wateja wengi zaidi.


Ameyasema hayo mapema wakati akifungua zoezi la usafi katika wilaya hiyo lililofanywa na benki ya KCB maeneo ya Mbagala Zakhiem, na kuwaomba watoe mikopo ya riba nafuu katika eneo hilo kwa kuwa lina wafanyabiashara wengi na wadogo wakiwa wanahitaji kupewa nguvu ili waweze kufikia malengo yao.


Lyaniva ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, aliipongeza Benki ya KCB kwa juhudi na kufanikisha kuwaleta wadau mbali mbali pamoja na wananchi wa Mbagala kushiriki katika kufanya usafi. “Mlichokifanikisha leo si kidogo na ninawapongeza lakini pia iwe chachu ya kutaka kufanya zaidi katika jamii yenu, ni mfano mzuri wa kuigwa hata na makampui mengine.” aliongeza DC Lyaniva.

Aliendelea kusema kuwa anafurahia kuona wawekezaji wengi wanaendelea kuwekeza katika wilaya ya Temeke kwani anategemea ubora wa huduma kwa wananchi wake, lakini pia watamsaidia katika shughuli nyingi za kijamii ikiwemo kujenga Madarasa, Zahanati na hata huduma za usafi katika maeneo hayo kwani ndio malengo ya serikali ya awamu ya tano.

Mkuu wa wilaya huyo aliendelea kusisitiza kuwa zoezi la usafi liwe ni endelevu kwani yeye anafanya usafi kila jumaa mosi na sio mpaka iwe jumaa mosi ya mwisho wa mwezi, lakini pia alisema anashukuru kupata wasaidizi kwani alikuwa akipata usumbufu mkubwa hasa katika eneo hilo la Zakiem.


Afisa Mazingira wa Wilaya ya Temeke, Ally Hatibu aliwashukuru wakazi wa Mbagala kwa kuitikia wito wa Benki ya KCB. Alisema ni ishara njema inayoonyesha kwamba wakazi wa hao wanalipa kipaumbele swala la kutunza mazingira.”Ninawasihi kuendeleza kuukuza ushirikiano huu na kufanya shughuli endelevu za kutunza mazingira.” alisema.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa KCB Benki Christina Manyeye alisema kuwa wameamua kufanya zoezi hilo ili kuonyesha ushirikiano kati yao na wafanyabiashara pamoja na wakazi wa maeneo hayo, japo kuwa ukiliangalia zoezi hilo kwa haraka haraka utaliona kama ni dogo lakini kwao lina maana kubwa sana.

Aliendelea kusema kuwa KCB Benki inaendelea kuwawezesha wafanya biashara wadogo wadogo katika maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi, kama leo ilivyotoa zawadi za vitendea kazi kwa wafanyabiashara wa eneo hilo kama miamvuli ya biashara na zawadi nyinginezo.

Hafla hiyo pia ilitoa fursa pekee kwa mama ntilie wanaofanya shughuli zao katika maeneo yanayozunguka Tawi la Benki ya KCB Mbagala, kwa kutoa huduma ya chakula kwa washiriki zaidi ya 100 katika hafla hiyo. “Kutoa fursa hii kwa akina mama hawa ilikuwa na jambo la kusudi na tuliwafuata bayana na kuwaomba kushiriki. Tutaendeleza ushirikiano wa aina hii kwa wajasiriamali wote wanaolizunguka tawi letu hasa wakina mama.’’ Alisema Bi. Christine Manyeye, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano ya Umma wa Benki ya KCB Tanzania.

Kwa upande wake, Bi. Jamila Dilunga ambaye alikuwa muwakilishi wa mama ntilie waliohudumia hafla hiyo, aliishukuru Benki ya KCB kwa fursa waliotoa kwa wakina mama wa Mbagala. Alisisitiza kwamba hakuna sababu ya Mbagala Zakhem kuwa chafu wakati washapata mdau kama Benki ya KCB anayejali mazingira na usafi wa eneo la biashara yake. Aidha, aliiomba Benki ya KCB kufanya swala la kuhamasisha usafi katika eneo hilo kuwa endelevu.


Na mwisho alipenda kutoa shukrani za dhati wadau waliofanikisha zoezi hilo kwenda mbele wakiwemo, Clouds Media Group, kampuni ya usafi ya West Pro, Creative Company, Pamoja na kampuni ya Proper Media.Benki ya KCB Tanzania, Jumamosi ya tarehe 8 Septemba imefanya shughuli za usafi ikishirikiana na wakazi wa Mbagala katika eneo la Mbagala Zakhem ambapo benki hiyo imefungua tawi lake la 14 nchini hivi karibuni.

Clouds Media Group, Green WastePro Limited, kampuni ya kazoa na kuchakata taka pamoja na The Creative Company, kampuni kutengeneza matangazo ndiyo walikuwa washirika wakuu wa Benki ya KCB Tanzania katika hafla hiyo iliyopokelewa kipekee na wakazi wa Mbagala ambao pia walishiriki. Hafla hiyo pia ilipewa uzito kwa kuwepo kwa ofisi za uongozi za Wilaya ya Temeke ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Afisa Mazingira na Watendaji wa Kata na mitaa.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke  Mh. Felix Lyaniva  akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya KCB Zuhura Muro(kulia)  wakifanya usafi na pamoja kwa ajili ya kuweka mazingira safi na salama Mbagala Zakhiem Jijini Dar es salaam.
Wafanyakazi wa  Benki ya KCB, wafanyabiashara wadogo wadogo, kampuni ya Green Waste wakiendelea na usafi Mbagala Zakhiem kwa ajili ya kuweka mazingira safi na salama.
Meneja Masoko wa KCB Benki Christina Manyeye akitoa zawadi kwa wafanyabiashara walioshirikiana nao katka zoezi la usafi wa mazingira Mbagala Zakhiem Jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad