HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 9 September 2018

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA APOKEA MISAADA YA KIBINADAMU YA WAFUNGWA GEREZA KUU KARANGA, MOSHI

Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike akisalimiana na Meneja Miradi wa Asasi ya Kidini ya New Life In Christ Ndg. Charles Shang’a mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga Moshi kwa ajili ya hafla fupi ya kupokea Misaada ya Kibinadamu iliyotolewa na Asasi hiyo kwa ajili ya wafungwa leo Septemba 8, 2018.

Na Deodatus Kazinja, Moshi

Wito umetolewa kwa Asasi mbalimbali za kiraia nchini kujitokeza kushirikiana na Jeshi la Magereza katika kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazoweza kulikwamisha katika kutoa huduma muhimu za wafungwa magerezani  kutokana na ufinyu wa bajeti. 

Hayo yamesemwa leo na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Phaustine Kasike katika hafla ya kupokea msaada wa Kibinadamu uliotolewa na Asasi ya Kidini ya New Life In Christ  iliyofanyika katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga mjini Moshi jana Septemba 8, 2018.

“Ni ukweli usiopingika kuwa Jeshi la Magereza limekuwa likishindwa kutekeleza kwa ukamilifu utoaji wa baadhi ya huduma muhimu kwa wafungwa kutokana na ufinyu wa bajeti.” Amesema Kamishna Jenerali Kasike.
Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike (wa pili kushoto) akipokea msaada wa vifaa vya kuchomelea akiwa ni sehemu ya vifaa vilivyotolewa na Asasi ya Kidini ya New Life In Christ kwa ajili ya wafungwa vitakavyotumika kuwafundisha stadi mbalimbali za ufundi magerezani. 

Jenerali Kasike ametoa wito kwa Asasi nyingine kuiga mfano uliooneshwa na New Life in Christ na Dorcas Aid International Tanzania zinavyoshirikiana na Jeshi la Magereza.

Asasi ya Kidini ya New Life In Christ  pamoja na Dorcas Aid International Tanzania kwa miaka 14 sasa tangu 2005 zimekuwa zikishirikiana na Jeshi la Magereza kwa kutoa misaada ya Kibinadamu na Kiroho yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.7 hadi hivi sasa.

Kwa kipindi chote hicho Asasi hizi zimekuwa zikitoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa semina za ushauri pamoja na mafunzo ya ufundi stadi kwa wafungwa na Maafisa wa Jeshi la Magereza.
Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike akipokea msaada wa vyerehani uliotolewa na Asasi ya Kidini ya New Life In Christ leo Septemba 8, 2018 kwa ajili ya wafungwa. Hafla ya upokeaji wa misaada hiyo imefanyika katika gereza Kuu Karanga Moshi.

Huduma nyingine ambazo zimewezeshwa na Asasi hizo ni kuwa na vituo vidogo vidogo vya kujifunza kufanya mambo ambayo tayari yanafanyika ndani ya magereza kama vile uokaji mikate, ushonaji na kudarizi, ushonaji wa viatu, ukinyozi, useremala na uchomeleaji mchanganyiko.

Katika hafla hiyo Asasi ya Kidini ya New Life In Christ imekabidhi msaada wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.2 ambapo wameahidi kuendelea kutoa misaada ya namna hiyo kwa kadiri Mungu atakavyowajalia.

Misaada ya Kibinadamu iliyotolewa leo imewalenga zaidi wafungwa walioko Mikoa ya  Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Mwanza.

Wakati huo huo,  Kamishna Jenerali Kasike amewaagiza wakuu  wote wa magereza yote ambayo vifaa hivyo vitapelekwa kuhakikisha wanavitunza na kuvitumia kwa uadilifu kama ilivyokusudiwa.
Wageni wa meza kuu wakiongzwa na Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike (katikati) wakiimba wimbo wa Taifa la Tanzania ikiashiria ufunguzi wa hafla fupi ya kupokea misaada ya Kibinadamu kwa ajili ya wafungwa iliyotolewa na Asasi ya Kidini ya New Life In Christ. Tukio hilo limefanyika leo Septemba 8, 2018 katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga Moshi.
Mkurugenzi wa Asasi ya Dorcas Aid International Tanzania Bi. Lilian Urasa akitoa maelezo mafupi kabla ya kukabidhi msaada wa Kibinadamu kwa ajili ya Wafungwa nchini. Dorcas Aid International Tanzania hushirikiana na Asasi ya Kidini ya New Life In Christ katika kutoa misaada ya namna hiyo.
Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike akitoa hotuba kwa wageni mbalimbali (hawapo pichani) waliohudhuria hafla fupi ya kupokea msaada wa Kibinadamu kwa ajili ya wafungwa kutoka kwa Asasi ya Kidini ya New Life In Christ leo Septemba 8, 2018 katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga Moshi.
Baadhi ya Maafisa na askari wa Ofisi ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro na Gereza Kuu Karanga wakifuatilia hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike (hayupo pichani) wakati wa hafla fupi ya kupokea msaada wa Kibinadamu kutoka kwa Asasi ya Kidini ya New Life In Christ leo Septemba 8, 2018 katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga Moshi.
Mwenekano wa baadhi ya misaada ya Kibinadamu iliyotolewa Asasi ya Kidini ya New Life In Christ iliyokabidhiwa kwa Jeshi la Magereza leo Septemba 8, 2018 katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga Moshi. Misaada iliyotolewa leo kwa ujumla wake ina thamani ya zaidi ya milioni 200.2.
Kikundi cha Sanaa cha Mama Jusi Anglikan cha mjini Moshi kilikonga nyoyo za wageni waalikwa katika hafla ya kupokea msaada wa Kibinadamu uliotolewa na Asasi ya Kidini ya New Life In Christ leo Septemba 8, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya askari wa magereza mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla ya kupokea misaada ya Kibinadamu kutoka kwa Asasi ya Kidini ya New Life In Christ leo Septemba 8, 2018. Kutoka kulia ni Miradi wa Asasi ya Kidini ya New Life In Christ Ndg. Charles Shang’a, Mkurugenzi wa Asasi ya Dorcas Aid International Tanzania Bi. Lilian Urasa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Dkt. Hasan Mkwiche. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Emmanuel Lwinga, Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Anderson Kamtiaro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Hamis Isaya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad