HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 20 September 2018

Jalada la kesi ya Uhujumu Uchumi dhidi ya aliyekuwa mfanyakazi wa TAZAMA lipo kwa DPP

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya  Uhujumu Uchumi dhidi ya aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia(Tazama), Samwel Nyakirang'ani na wenzake, umeieleza mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa (DPP), kwa ajili ya kulipitia na kulifanyia uchambuzi.

Imedaiwa, DPP analichambua kwa ajili ya kuangalia washtakiwa gani washtakiwe na washtakiwa gani waachiwe huru.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Patrick Mwita, ameeleza hayo leo Septemba 19, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Amedai, amewasiliana na wenzake na  wamemueleza kuwa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha uchambuzi, akaiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi tarehe nyingine

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote , aliutaka upande wa mashtaka kuharakisha zoezi la uchambuzi ili haki iweze kupatikana.

kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 3, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa na kuangalia kama uchambuzi huo umekamilika.

washtakiwa  wengine katika kesi  hiyo ni Nyangi Mataro mwalimu wa shule ya msingi Ufukoni na mkazi wa Kisiwani Mkajuni Kigamboni.

Mfanyabaishara, Farijia Ahmed mkazi wa Soko Maziwa Kigamboni, Malaki Mathias, mkazi wa Magogoni, Kristomsi Angelus, mkazi wa Soko Maziwa,  Fundi Ujenzi Pamfili Nkoronko, mkazi wa Tungi Kasirati na Henry Fredrick, mkazi wa Tungi Kigamboni.

Wengine ni Audai Ismail ambaye ni mkazi wa Kibaha, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwa  kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, kinyume cha sheria  ya Uhujumu uchumi.

Inadaiwa, kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 huko Tungi Muungano wilaya ya Kigamboni, washtakiwa kwa pamoja walijiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoa katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Bandari nchini(TPA).

Pia wanadaiwa  kutoboa  bomba  hilo ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta,  mali ya (TPA).

Aidha wanadaiwa kuharibu  bomba la mafuta mazito lenye upana wa Inchi 28, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi, mali ya (TPA).

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad