HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 25 September 2018

DAWA YA MATAPELI WANAOUZA NYUMBA NA MALI ZA RAIA KINYUME NA SHERIA YAPATIKANA

* MAKONDA AALIKA WANANCHI UZINDUZI WA FLYOVER 

Na Leandra Gabriel, blogu ya jamii
MKUU wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Paul Makonda leo amekutana na wawakilishi wa  benki, wenyeviti wa mitaa, madalali wa mahakama na kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti wizi na utapeli ambao umekuwa chanzo cha maumivu kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho Makonda amewataka watu wa benki kuhakikisha wanafanya uchunguzi na kujiridhisha kabla ya kutoa mkopo na hii ni baada ya kuibuka kwa utapeli wa watu kutumia hati za watu na kuchukuwa mkopo pasipo muhusika kujua jambo linalopelekea nyumba na Mali za watu kupigwa mnada na kuacha familia zikikosa makazi. 

Aidha  Makonda amewataka madalali wa mahakama na wale wa benki kuhakikisha wanatoa taarifa kwa mkuu wa wilaya na mwenyekiti wa mtaa kabla ya kufanya mnada huku akiwaagiza kuhakikisha wamesajiliwa na kuwa ndani ya chama cha madalali ili kuondokana na uvunjifu wa amani wakati wa minada. 

Pamoja na hayo  Makonda amewataka wenyeviti wa mitaa kusimamia sheria na taratibu kwa kuhakikisha minada inafanyika pasipo uonevu wala uvunjifu wa amani. 

 Makonda pia amewaagiza watu wa benki kuhakikisha maafisa mikopo na wanasheria wao wanazingatia taratibu baada ya kubaini baadhi yao wamekuwa chanzo cha migogoro na utapeli.

Pia  Makonda amewapa mwezi mmoja watu wa benki, Wenyeviti wa mitaa, Madalali wa mahakama na benki kuandika changamoto na mapendekezo yao kisha kuyawasilisha kwake kwaajili kufanyiwa marekebisho  mwisho wa siku wawe na sheria nzuri inayomlinda mkopeshaji na mkopwaji.

Hata hivyo, Makonda amewataka wote wanaokopesha wananchi mitaani kienyeji pasipo kusajiliwa wala kuwa na vibali vya utambuzi kuacha Mara moja kwakuwa wamekuwa chanzo cha migogoro huku akiwataka madalali wa nyumba,viwanja na mashamba kuhakikisha wanasajiliwa na kutambulika na serikali.

Mwisho amewataka wananchi na viongozi mbalimbali bila kujali itikadi wala vyama wa Mkoa wa  kujitokeza kwa wingi siku ya Alhamisi katika makutano wa barabara ya Tazara kushuhudia uzinduzi wa Flyover itakayozinduliwa na Rais John Magufuli.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda akizungumza na  wanasheria,madalali wa Mahakama pamoja Benki  ambapo amewataka watu wa Benk kuhakikisha wanafanya uchunguzi na kujiridhisha kabla ya kutoa mikopo.(Picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii)
 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda akiangalia nyaraka mbalimbali.
Mkutano ukiendelea.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad