
Na Karama Kenyunko,Globu ya jamii
MSHITAKIWA Harbinder Singh Sethi anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ana miezi sita sasa hajawahi kuonana na mke wake.
Sethi ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi wakati kesi yao ilipokuja kwa kutajwa.
Ameeleza hayo, baada ya Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono kuieleza Mahakama kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine.
Kutokana na maelezo hayo kutoka kwa Kombakono Wakili anayemtetea Sethi, Dorah Mallaba alidai kuwa bado hawajapata kibali kwa ajili ya mshtakiwa Sethi kuonwa na mkewe.
Kutokana na hayo, aliiomba Mahakama iruhusu japo kwa dakika tano Sethi aonane na mkewe.
"Naomba Mahakama itumie busara kwa kuwa make wake yupo hapa mahakamani," amesema.
Wakili Kombakono alipinga hoja hiyo ya wakili Mallaba na kueeleza kuwa taratibu za kuwaona mahabusu zifuatwe.
Hata hivyo, Hakimu Shahidi amewaeleza upande wa utetezi kuwa taratibu za kuwaona na kuwatunza mahabusu ipo chini ya Magareza hivyo, kama kuna jambo lolote mahususi walete mahakani.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 13 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Katika kesi hiyo Sethi anashtakiwa pamoja na James Rugemarila, ambapo wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.
No comments:
Post a Comment