HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 13, 2018

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC wafunguliwa mjini Windhoek, Namibia

Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) umefunguliwa rasmi katika Hoteli ya Safari mjini Windhoek, Namibia tarehe 13 Agosti 2018.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga ambaye ameambatana na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania ambao ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda; Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (anayesimamia masuala ya Ujenzi) Mhandisi Joseph Myamhanga, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa; Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu na Naibu Katibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin Paul Mhede

Mkutano huu ni sehemu ya mikutano ya awali ya maandalizi ya mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 17 na 18 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia. Mikutano mingine ya awali ni mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC uliofanyika tarehe 9 na 11 Agosti 2018 na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa , Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Kanda kwa kipindi cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018.

Mkutano wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utapokea, kujadili na kutolea maamuzi ya mapendekezo mbalimbali yanayotokana na mikutano ya kisekta na kamati za jumuiya kwa kipindi cha mwaka 2017/18. Pamoja na mambo mengine mkutano huu;

Utafanya uteuzi wa Mwenyekiti wa SADC na inatarajiwa kuwa Jamhuri ya Namibia ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha 2018/2019. Nafasi ya Makamu mwenyekiti itajazwa pia na nchi itakayoteuliwa ambayo itajulikana tarehe 17Agosti 2018.

Uteuzi wa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Inatarajiwa kuwa Jamhuri ya Zambia, ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha 2018/2019. Hivi sasa Tanzania ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake kwenye Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security).

Mambo mengine yanayotarajiwa kujitokeza na kujadiliwa katika mkutano huu ni pamoja na; masuala ya fedha; Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Viwanda wa SADC (Report on the operationazaition) na Maendeleo ya Viwanda; Kutia saini itifaki mbalimbali ikiwa ni pamoja na itifaki ya Kulinda Hakimiliki ya Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea ya mwaka 2017. Pia Mkutano huu utatoka na tamko la nchi wanachama wa SADC la kutokomeza malaria katika ukanda wa SADC ifikapo mwaka 2030.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika unaofanyika tarehe 13 na 14 Agosti 2018 katika hoteli ya Safari mjini Windhoek, Namibia .
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena L. Tax (mstari wa mbele kati) akiwa katika picha ya pamoja na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika mara baada ya hafla ya ufunguzi wa mkutano huo mjini Windhoek, Namibia.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, Dkt. Stergomena L. Tax akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa Mawaziri wa SADC.

Katika hotuba yake aliwasilisha taarifa fupi ya mwaka ya utekelezaji ya Jumuiya hiyo pamoja na kuishukuru Serikali ya Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda) kwa uongozi na usimamizi mzuri katika kipindi chote cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Mhe Dkt. Lindiwe Sisulu (kushoto) akikabidhi nafasi ya uenyekiti kwa mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwa.
Mwenyekiti mpya wa Mawaziri wa SADC, Mhe. Nandi-Ndaitwa akihutubia mara baada ya kupokea nafasi hiyo.
Katika hotuba yake alisistiza umuhimu wa kuwawezesha vijina kwa kuwa ndio nguzo kuu katika kuinua uchumi wa taifa lolote duniani sambamba na uwekezaji katika viwanda. Pamoja na hayo akaeleza malengo makuu ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuondoa umasikini na kuinua uchumi ndani ya kanda.
Mkutano ukiendelea, walioketi nyuma ya Mhe. Waziri Mahiga kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Prof. Adolf Mkenda na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Viwanda na Mawasiliano (anayeshughulikia masuala ya ujenzi) Mhandisi Joseph Nyamhanga.
Mkutano ukiendelea, Kutoka Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Innocent Shiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin Mhede.
Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylivester Ambokile na wajumbe wengine wa Serikali ya Tanzania wakifuatilia ufunguzi wa mkutano.
Sehemu nyingine ya wajumbe kutoka Serikali ya Tanzania wakifuatilia mkutano.
Balozi wa Namibia nchini Tanzania pamoja na wajumbe wengine wa mkutano huo wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad