Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Delila
Kimambo akielezea jinsi mashine ya kupima moyo (Echocardiogram) inavyofanya
kazi ya kutambua matatizo yaliyopo katika moyo wakati wa mkutano wa kwanza
wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika leo katika ukumbi
wa mikutano wa JKCI uliopo Jijini Dar es Salaam.
Na Salome Majaliwa - JKCI
Madaktari wa Hospitali za Rufaa nchini wameshauriwa kuwatuma
mapema wagonjwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pindi
wanapowapima na kugundulika kuwa na ugonjwa huo ili waweze kupatiwa
matibabu mapema.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari
bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka JKCI Delila Kimambo wakati wa mkutano
wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo.
Dkt. Delila alisema wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Hospitali mbalimbali
hapa nchini rufaa yao huwa ni Taasisi ya Moyo hivyo basi ni muhimu wagonjwa
hao wakafika katika Hospitali hiyo kwa wakati.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani Prof.Matthew Sackett akielezea jinsi mtambo wa Cathlab unavyotumika kutibu na kupima magonjwa ya moyo wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.
“Wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao huwa imechoka, kama wagonjwa
hawa wangefika mapema kwetu wangepata matibabu madogo kuliko kupatiwa
matibabu makubwa ya upasuaji wa kifua au bila kufungua kifua kwa kutumia
tundu dogo”.
“Kutokana na wagonjwa wengi kuchelewa kufika hospitalini ama kutokupata
matibabu ya moyo kwa wakati, tumeona tuwe na mafunzo haya hii itawasaidia
madaktari wengi kupata ujuzi zaidi na kuweza kutambua wagonjwa kwa wakati”,
alisema Dkt. Delila.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo Dkt. Delila alisema lengo ni kuwapatia
madaktari ujuzi hususani wa namna ya kupima moyo kwa kutumia mashine za
ECHO na umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG).
Kwa upande wake Daktari kutoka hospitali ya Amana Natalius Kapilima alisema
mafunzo hayo yamewasaidia kupata ujuzi utakaowawezesha kuwatambua
wagonjwa wa moyo kupitia vipimo vya ECHO na ECG.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka hospitali ya Aga Khan Prof.
Mustafa Bapuma aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kuona mbali na
kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo kwa madaktari. Kupitia mafunzo hayo
wataweza kutibu wagonjwa wa moyo kwa ustadi na ufanisi zaidi kuliko hapo awali.
Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa
kushirikiana na Kampuni ya Merck ambapo jumla ya washiriki 80 kutoka Hospitali
mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam walishiriki.
Baadhi ya Madaktari wa Magonjwa ya Moyo kutoka Hospitali
mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia mada ya jinsi ya kumtambua
mgonjwa mwenye matatizo ya moyo kwa kupitia kipimo cha ECHO wakati wa
Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini
uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.
Picha na Genofeva Matemu - JKCI
No comments:
Post a Comment