HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 12 August 2018

ASASI ZA KIRAIA ZAOMBWA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI KUTATUA CHANGAMOTO MBALIMBALI


Asasi za kiraia zimeombwa kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa upatikanaji wa huduma ya maji. 

Diwani wa Kata ya Kwembe wilayani Ubungo, Dweza Kolimba amesema asasi za kiraia zina nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika jamii kwa kushirikiana na wananchi na watendaji wa serikali. 

Akizungumza katika semina iliyoandaliwa na asasi ya Pakacha kwa ajili ya kujadili utatuzi wa changamoto ya maji, kuanzia ufuatiliaji wa rasilimali fedha na utekelezaji wake, Kolimba amesema upatikanaji wa maji katika kata yake umekuwa wa shida, hivyo kupitia asasi kama ya Pakacha, wananchi wanaweza kuelimishwa kushirikiana na viongozi ili kutatua kero hizo. 

Amesema upatikanaji wa maji umekuwa wa shida katika kata yake, huku akisema kuwa wananchi wengi watapata maji baada ya mradi mkubwa wa Luguruni kukamilika. “Tayari mabomba yamesambazwa, hivyo tunaomba mradi huu uishe mapema ili watu wapate maji,” amesema Kolimba. Everyline Francis, mjumbe wa kamati ya maji ya Kata ya Kwembe amesema jamii ipewe elimu ya kutunza vyanzo vya maji na kuzuia uharibifu wa mazingira. 

Upatikanaji wa maji umekuwa na changamoto katika kata za Kwembe, Msigani na Kibamba, hivyo asasi ya Pakacha, kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society kulazimika kutoa elimu kwa wananchi juu ya ufuatiliaji na utunzaji wa vyanzo vya maji. 

Akizungumza kwa niaba ya Mhandisi wa maji wa Manispaa ya Ubungo, Hamad Sendekwa amesema ameomba wananchi washirikiane na watendaji ili kutatua kero za maji na jitihada zinaendelea kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana wakati wote. Alisema ushirikiano huo utasaidia kuibua changamoto zinazokwamishwa na rasilimali fedha au kutowajibika kwa baadhi ya watendaji. 

Alisema asasi zinaweza kuleta mabadiliko kwa kufuatilia miradi ya maji, ambayo inakwamishwa kwa sababu mbalimbali na kuwaelimisha wananchi jinsi ya kulinda miundo mbinu ya maji na ufuatiliaji wake. Katibu wa Pakacha, Haroun Jongo amesema lengo la semina hiyo ni kutoa msukumo kwa utelekezaji wa miradi ya maji kwa kuibua hoja kwa wananchi, kwa lengo moja tu, kuleta maendeleo. 

Amesema lengo la semina hiyo ni kuleta jukwaa la majadiliano kati ya viongozi, wananchi na watendaji wa serikali za mitaa ili kutatua kero za maji kwa wananchi kupitia mfumo wa Pets. Pets ni mfumo unaowezesha ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma zinazotoka Serikali Kuu au halmashauri kwa maendeleo ya wananchi kuanzia ngazi za mitaa hadi kata na kuendelea. 

Mwezeshaji, Enock Daniel Kijo akitoa mafunzo kwa washiriki wa semina ya maji iliyoandaliwa na asasi ya Pakacha Group kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society kwa kata za Kwembe, Msigani na Kibamba za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. 

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad