HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 17 July 2018

TAMWA, MASHIRIKA YA CANADA,ULAYA WAZINDUA FILAMU INAYOHUSU KUPINGA UKEKETAJI


Na Khadija Seif , Globu ya jamii   
CHAMA cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kutoka nchini Canada na mataifa ya Ulaya wamefanya uzinduzi wa filamu inayohusu maisha ya binti wa kike inayojulikana kama  In the name of your daughter.

Uzinduzi wa filamu hiyo umefanyika jana katika ukumbi wa Alliance Francie's jijini dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa  ndani na nje ya nchi.

Filamu hiyo inazungumzia maisha ya watoto wa familia zenye utamaduni wa ukeketaji hasa mkoani Mara wakiwa bado wanaendelea na mila hiyo potofu inayowakandamiza  watoto wa Kike kwakuwa  hawajapata elimu ya kutosha kuhusu athari zake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwakilishi kutoka Serikalini   Grace Mwangwa  amesema jamii bado zinahitaji elimu ya kutosha ili kupiga vita dhidi ya ukeketaji na kwamba Serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na mashirika ili kumkwamua mtoto wa kike kufikia malengo yake.

Mwangwa amesema baadhi ya jamii  wameichukulia  desturi hiyo kama  sheria kwao na watoto wengi hunyanyasika pindi wanapokataa kufanyiwa kitendo hicho na hata kutengwa na jamii kabisa .

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA  Edda Sanga  amesema  chama chao kimefanya juhudi na jitihada na kuona kwa namna moja au nyingine kushirikiana na vyombo vya habari kutokomeza vita hiyo ya ukatili wa kijinsia.

"Kwani kwa kiwango kikubwa mpaka sasa ndoa za utotoni zimepungua kutokana na elimu kufika sehemu mbalimbali pamoja na madhara yake kubainishwa  na kuwepo kwa Sheria kali kwa wanaojihusisha na uhalifu huo wa kumnyima haki za msingi mtoto wa kike,"amesema.

Pia ameeleza kuwa  vituo vya kuhifadhi wahanga hao hasa watoto wa kike vilijengwa kwa ajili yao kutokana na kutengwa na familia zao na kubaki wakizurura maporini ambapo yanahatarisha maisha yao endapo watakutana na wanyama wakali au hata kujiingiza kwenye ulawiti au kubakwa .

Wakati huo huo Mratibu wa Save House Robi Samweli amesema anashirikiana pia  na  dawati la jinsia ,mwenyekiti wa mtaa ,Ofisa ustawi na Jeshi la polisi kukamata wahalifu wanaojihusisha na ukatili huo.

"Kushirikiana na mashirika mbalimbali tumeweza kujenga nyumba hizo kwa ajili ya kuwahifadhi ili kuwanusuru kwenye janga hilo,na watoto wameonyesha muamko kwani baadhi yao yameweza kuja pasipo kushawishiwa na mtu na wengine kubaki kuishi hapo kutokana na kutoamini tena familia zao," amesema.

Anafafanua zaidi imani zilizojengeka na sababu zinazowasabisha watoto hao kufanyiwa hivyo ni pamoja na kujipatia utajiri pindi msichana husika anapoolewa kwani msichana aliyefanyiwa kitendo hiko anapewa ng'ombe 10 hadi 11. Wakati msichana ambae hajafanyiwa hupewa ng'ombe saba.

Hata hivyo watoto wengi wanakosa amani mashuleni kwani wanaingia kwenye wakati mgumu wa kufikiria wakati wowote watafanyiwa kitendo hiko. Na baadhi ya familia wamekua wakiwatia hofu watoto hao na kuwatenga kuwa endapo hawatokeketwa hawataweza kuishi tena kwenye familia zao.
  Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA  Edda Sanga akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa filamu ya "In The Name of Your Daughter" inayohusu ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike katika Ukeketaji.
Baadhi ya waalikwa wakifuatilia filamu hiyo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad