HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 13 July 2018

JWTZ YAMTAKA ALIYELALAMIKIA HUDUMA HOSPITALI YA LUGALO AJITOKEZE KUBAINI UKWELI VINGINEVYO WATAMSAKA

Na Luteni  Selemani Semunyu
Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania limekanusha taarifa zilizosambazwa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko juu matibabu  ya mtoto anayedaiwa kuvunjika na kupatiwa  huduma  katika Hospitali kuu ya jeshi ya Lugalo.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo  Jijini  Dar es Salaam msemaji mkuu wa Jeshi Kanali Ramadhani Dogoli alimtaka aliyejinasibisha kama mlalamikaji kuwasilisha malalamiko yake kama yana ukweli ili hatua zichukuliwe kwa wahusika.

“ Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania JWTZ linamtaka malalamikaji alete taarifa kwenye uongozi ili kama matukio hayo yametokea tuweze kuchukua hatua kwa wahusika” Alisema kanali Dogoli.

 Aliongeza kuwa iwapo aliyedai kulalamika atashindwa kufanya hivyo jeshi litaaamini kuwa mlalamikaji alikusudia kuichafua hospitali yetu kwa maslahi binafsi  na kwa sababu hiyo tutamtafuta haraka na kumchukulia hatua zinazomstahili.

Msemaji huyo wa JWTZ Mnamo Julai 10 mwaka huu ilisambaa habari ikilalamika huduma zisizoridhisha  katika kitengo cha mifupa katika hospitali ya lugalo  baada ya kudai  mtoto wake mkono umeunga vibaya na kutakiwa kupatiwa matibabu tena.

Hata hivyo alisema baada ya kupata taarifa walifanya uchunguzi ambapo yalipitiwa majina ya watoto wote waliotibiwa tangu April hadi 30 Juni mwaka huu hakuna mtoto aliyefika mara mbili kwa waliopata mivunjiko.

“ Watoto wawili tu ndio walitibiwa na wazazi wao walithibitisha kuwa maendeleo yao ni mazuri majibu yalipelekea kubaini kuwa labda muhusika alikusudia kuichafua Hospitali yetu” Alisema kanali Dogoli.

Kwa upande wake Mkuu wa tiba wa JWTZ Meja Jenerali Dk Denis Janga alisema amesikitishwa na taarifa hiyo ambayo pia imewagusa wataalam wa hospitali hiyo ambayo imekuwa ikitoa huduma kwa wananchi tofauti na majeshi mengine ambapo hospitali za jeshi zinahudumia wanajeshi na Familia zao pekee.

Alisema wataalam wa hospitali hiyo ni wataalam kama watalaaam wengine waliopata mafunzo ndani na n je ya nchi kama ilivyo wataalam wengine na kamwe hawatokatishwa tamaa na maneno ya kuichafua hospitali hiyo.

Mkuu huyo wa Tiba jeshini alisema wameapa kuilinda na kuitetea katiba na wamejitolea kuwahudumia watanzania hivyo hawatosita kufanya hivyo kwa moyo wao wote.

“ Kamwe hatutasita kuwahudumia Watanzania  kwa maneno ya uongo na kuwataka watanzania kuwapuuza watu wenye mtazamo wa kuwagombanisha na wananchi na sasa ni wakati wa kutiana moyo kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali” Alisema Meja Jenerali Janga .

Hospitali za Jeshi nchini ikiwemo  Hospitali kuu ya jeshi Lugalo  zimekuwa zikishiriki katika utoaji wa huduma kwa Wananchi kwa Zaidi ya ya asilimia 70 ukilinganisha na idadi ya Askari na wategemezi wao wanaopata huduma katika hospitali hizo.
 Msemaji Mkuu wa Jeshi Kanali Ramadhani Dogoli ( Wapili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu malalamiko ya uzushi dhidi ya Hospitali kuu ya Jeshi Lugalo wapili kulia ni Mkuu wa Tiba Jeshini Meja Jenerali Denis Janga na wakwanza kulia ni Mkuu wa Hospitali ya Lugalo Brigedia Gabriel Muhdize leo  Jijini Dar es Salaam (Picha na Luteni Selemani Semunyu)
Moja ya majengo ya Hospitali Kuu ya jeshi ya Lugalo ambayo imekuwa ikitoa huduma kwa wananchi raia kwa Asilimia 70 ukilinganisha na Wanajeshi  na Familia Zao wanaofika kutibiwa katika Hospitali hiyo( (Picha na Luteni Selemani Semunyu)  

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad