HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 17, 2018

Balozi Seif Ali Iddi afanya mazungumzo nauongozi wa STL Group

Uongozi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kitaalamu inayosimamia makampuni sita yanayojihusisha na masuala ya Miundombinu, Afya, Elimu, Biashara, Umeme na Mawasiliano ya Kisasa-STL Group imeonyesha nia ya kutaka kuiunga mkono Zanzibar ili iweze kuongeza nguvu za uwezeshaji katika kubuni mbinu na maarifa kwenye Sekta tofauti.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Amand Group iliyo chini ya Taasisi hiyo Bw. Nadas Simhoni aliyeuongoza ujumbe wa viongozi wanne wa Kampuni hiyo alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Bw. Simhoni alisema Amand Group yenye wataalamu wa kutosha ambao tayari wanawajibika katika mataifa ya Ghana, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Togo, Ivory Coast na Tanzania wana uzoefu mkubwa wa kusarifu mambo tofauti ikiwemo michoro ya majengo mbalimbali.

Alisema miradi ya maendeleo ya sekta za Elimu, Afya na Kilimo ambazo huijumuisha Jamii ndiyo vipaumbele vikubwa walivyoviangalia zaidi ambavyo utekelezaji wake hujumuisha jamii katika ngazi ya Kitaifa na Jumuiya za Kijamii.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia uongozi wa taasisi hiyo ya STL Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuipatia ushirikiano taasisi hiyo katika azma yake ya kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar.

Hata hivyo Balozi Seif aliuambia uongozi wa taasisi hiyo kwamba serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa tenda pale inapotaka kuanzisha miradi yake ya kiuchumi na ya kijamii jambo ambalo uongozi huo una fursa ya kuomba tenda hizo zinapotokea.

Taasisi ya kimataifa ya kitaalamu ya STL Group inasimamia Makampuni Sita yanayojihusisha na masuala ya Miundombinu ya Ujenzi, Sekta za Afya, Elimu, Biashara, umeme, Mafuta, Gesi pamoja na Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa .

Makampuni hayo ni pamoja na Super Tech Limited, Amand Energy, Amand, Agritop Limited, Super Lock pamoja na SAF STL Amand.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Amand Group iliyo chini ya Taasisi ya STL Group Bwana Nadas Simhoni(kulia) aliyeongozana ujumbe wa viongozi wanne wa Kampuni hiyo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (katikati) akizungumza na uongozi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kitaalamu inayosimamia Makampuni Sita yanayojihusisha na masuala ya Miundombinu, Afya, Elimu, Biashara, Umeme na Mawasiliano ya Kisasa ya STL Group huko Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad