HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 18 June 2018

Upinzani Wapongeza Juhudi za Serikali Kukuza Uchumi

Na Jonas Kamaleki-MAELEZO, Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum, Chama cha Wananchi (CUF), Mhe.Rukia Kassim amepongeza juhudi za Serikali katika kukuza uchumi ikiwemo kuongezeka kwa pato la Taifa.

Mhe. Rukia ameyasema hayo leo Bungeni, Jijini Dodoma wakati akichangia mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19.

“Naipongeza Serikali kwa hatua za kukuza uchumi  hasa ukuaji wa Pato la Taifa unaotarajiwa kuwa asilimia 7.2”, alisema Rukia.

Naye Mbunge wa Urambo, Mhe. Margreth Sitta ameipongeza Serikali kwa kupendekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike.

“Mheshimiwa Spika hatua hii ya kusamehe kodi hiyo itapunguza bei ya taulo hizo ambayo itawafanya wanafunzi wa kike kuzipata kwa bei nafuu na kuwawezesha kuhudhuria masomo kwa muda wote wa masomo ikilinganishwa walivyokuwa wakishindwa kufanya hivyo wakiwa katika siku zao kwa kukosa taulo”,alisema Mama Sitta.

Akichangia kwenye bajeti kuu ya Serikali, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Peter Serukamba amesema kuwa anampongeza saa Rais John Pombe Magufuli kwa kujenga miradi mikubwa miwili ya Standard Gauge naye Umeme wa Stiegler’s Gorge.

“Historia itamwandika Rais Magufuli kwa kazi kubwa anazofanya hasa kwa ujenzi wa miradi mikubwa nchini, ule wa reli ya Kisasa (Standard Gauge) na ule umeme wa Stiegler’s Gorge”, alisema Serukamba.

Aliongezea kuwa bajeti hiyo ni nzuri sana na inapaswa kuungwa mkono kwani inawajali wananchi.

Wabunge wanaendelea kuchangia bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 ambayo iliwasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai (Mb), akizungumza wakati wa kikao cha 52 cha Bunge la 1 leo tarehe 18 Juni, 2018 Jijini Dodoma.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Hawa Ghasia akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 wakati wa kikao cha 52 cha Bunge la 11 leo tarehe 18 Juni, 2018 Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akijibu swali wakati wa kikao cha 52 cha Bunge la 11 leo tarehe 18 Juni, 2018 Jijini Dodoma.
 Mbunge wa Jimbo la Missungwi mkoani Mwanza, Mhe. Charles Kitwanga akichangia hoja kuhusu taarifa ya hali ya uchumi na mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2018/19 wakati wa kikao cha 52 cha Bunge la 11 leo tarehe 18 Juni, 2018 Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akiteta jambo na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Singida, Martha Mlacha wakati wa kikao cha 52 cha Bunge la 11 leo tarehe 18 Juni, 2018 Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Seriikali za Mitaa (OR -TAMISEMI), Mhe. Joseph Kakunda akijibu swali wakati wa kikao cha 52 cha Bunge la 11 leo tarehe 18 Juni, 2018 Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango(kulia)na Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji wakifuatilia hoja za wabunge kuhusu taarifa ya hali ya uchumi na mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2018/19 wakati wa kikao cha 52 cha Bunge la 11 leo tarehe 18 Juni, 2018 Jijini Dodoma. (Picha zote na: Frank Shija - MAELEZO, Dodoma)

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad