HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 27 June 2018

SEKTA YA KILIMO ZANZIBAR YAENDELEA KUKUA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uagizaji wa baadhi ya bidhaa zikiwamo za chakula na Matunda nje ya Zanzibar umepungua kutokana na hamasa kubwa walionayo wananchi hasa wakulima katika muelekeo wa kuwekeza zaidi kwenye sekta ya Kilimo.

Alisema Sekta ya Kilimo ni miongozi mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Chama Cha Mapinduzi wakati kilipoomba ridhaa ya kutaka kuongoza Dola kwenye kampeni za uchaguzi mkuu kilipokuwa kikitangaza Sera na Ilani yake.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kuli hiyo wakati alipofanya mahojiano maalum na Timu ya Wanahabari wa Redio Uhuru pamoja na Magazeti ya Chama cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo waliotaka kujua utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwenye Ofisi ya Uratibu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Jijini Dar es salaam.

Alisema kutokana na Serikali za CCM kusamehe ushuru wa forodha kwa vifaa vya kilimo vinavyoingizwa nchini sambamba na kuendeleza mafunzo ya kisasa kwa wadau wa kilimo, wakulima wengi nchini hasa wale wanaojishughulisha na kilimo cha matunda wameongeza mara dufu uwezo wa uzalishaji.

Balozi Seif alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wakulima wengi wamekuwa wakilalamikia ufinyu za soko la bidhaa wanazozalisha jambo ambalo limefikisha baadhi ya bidhaa hizo kusafirishwa kupelekwa upande wa Tanzania Bara.

Alisema hatua hiyo imeonyesha mabadiliko makubwa yaliyokuwa yamezoelekea kwa muda mrefu katika kushuhudia bidhaa nyingi hasa zile za nafaka, mizizi, mboga mboga pamoja na matunda ziliingizwa Zanzibar zikitokea mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba kwa vile kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa, Wananchi na hasa Wakulima wanapaswa kuendelea kuzalisha mazao yao katika kiwango kinachokubalika kitaalamu ili Taifa liendelee kupunguza kasi ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Balozi Seif alisema Serikali imelazimika kufidia pembejeo kwa wakulima na kupunguza bei ya dawa ili kuhamasisha wananchi walio wengi zaidi na vijana kuelekeza nguvu zao katika sekta ya kilimo yenye uwezo wa kutoa ajira pana zaidi na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa.

Akizungumzia juu ya sekta nyengine za kiuchumi alitoa mfano " sekta zile za Utalii, Viwanda, Elimu, Afya pamoja na Miundombinu ya Mawasiliano ya Barabara na Anga chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein zimeweza kupiga hatua kubwa katika uimarishwaji wa Miundombinu kwenye maeneo hayo". Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema.

Alisema ujenzi wa eneo la maegesho ya ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Gati ya Malindi na baadhi ya Barabara zinazoelekea katika maeneo ya Utalii ni mfano hai unaothibitisha utekelezaji wa kasi wa Ilani na Sera ya CCM ya Mwaka 2015/2020 uliofanikiwa ndani ya Miaka Mitatu.

Balozi Seif aliieleza Timu hiyo ya Wanahabari wa Redio Uhuru na Magazeti ya Chama ya Uhuru na Mzalendo kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kupokea watalii zaidi ya laki 500,000 ifikapo Mwaka 2020 na lengo hilo linaanza kutoa sura nzuri zaidi kwa vile hivi sasa inakadiriwa kufikia zaidi la Laki 350,000.

Kwa upande wa makusanyo ya mapato Balozi Seif alisema yapo mafanikio makubwa yiliyofikiwa kutokana na Serikali Kuu kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali.

Alisema hatua hiyo imeisababishia Serikali kupitia taasisi zake kukusanya Mapato yanayokadiriwa kufikia shilingi Bilioni 400,000/- lengo likiwa kuondokana na utegemezi ambao kwa sasa umefikia asilimia 7% kutoka asilimia 20% katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2016.

Balozi Seif alifahamisha kwamba myanya ya rushwa imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali, Taasisi za Umma pamoja na wananchi wazalendo.

Aidha kwa upande wa amani na utulivu wa Taifa, Balozi Seif kupitia kipindi hicho Maalum cha Mahojiano aliwasihi Wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar kuendelea kuitunza lulu hiyo iliyo adimu kupatikana katika baadhi ya mataifa mengi Duniani yakiwemo yale ya Bara la Afrika.

Alisema viongozi wakuu kwa kushirikiana na wasaidizi wao wamekuwa mstari wa mbele katika kusisitiza Jamii kudumisha amani na utulivu ambayo ndio ngao kubwa ya kuendeleza mshikamo uliojengeka kwa Watanzania walio wengi mijini na vijijini.

Alikumbusha kwamba Serikali zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kusimamia ulinzi wa amani iliyopo nchini muda wote hata wakati unapowadia wa Taifa linapongia katika harakati za Uchaguzi Mkuu ambazo huonekana baadhi ya wafuasi wa Vyama vya Siasa wakati mwengine hujaribu kuitikisha amani hiyo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa Mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bibi Justa Matari Nyange Ofisi ya Uratibu wa SMZ Jijini Dar es salaam.

Katika Mazungumzo yao Viongozi hao walizungumzia hatua zinazoendelea katika maandalizi ya ushiriki wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Guangzhou Nchini China mnamo Mwezi wa Septemba Mwaka huu.

Balozi Seif alimueleza Mkurugenzi huyo wa Asia kwamba Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa mshirika mkubwa wa Tanzania katika masuala ya Utamaduni, Biashara pamoja na Historia mara tu baada ya Uhuru wa Tanganyika 1961 na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Alisema uhusiano huo unaimarika kupitia mialiko na muingiliano wa ziara za mara kwa mara za pande hizo mbili, alisisitiza kwamba ni vyema vikaendelea kujengewa mazingia ya kuimarishwa siku hadi siku kwa faida ya jamii ya sasa na ile ijayo ya pande zote mbili.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bibi Justa Matari Nyange alisema kwa vile kamati za maandalizi ya Maonyesho hayo chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zimeshaundwa kwa sehemu zote mbili, ipo haja ya kukutana pamoja katika njia ya kupata mafanikio ya jumla. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akifanya mahojiano maalum na Wanahabari wa Redio Uhuru pamoja na Magazeti ya Chama cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo waliotaka kujua utekelezaji wa ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwenye Ofisi ya uratibu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bibi Justa Matari Nyange Ofisi ya Uratibu wa SMZ Jijini Dar es salaam. Mazungumzo hayo yalijikita katika kuangalia hatua zinazoendelea katika maandalizi ya Ushiriki wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Guangzhou Nchini China mnamo Mwezi wa Septemba Mwaka huu.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad