HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 8, 2018

MPANGO WA MATIBABU KUPITIA CHF ILIYOBORESHWA KUANZA KARIBUNI

*Katibu wa afya Dar, Wizara wazungumzia mafunzo waliyotoa kwa watumishi ili kuufanikisha mpango huo

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
MPANGO wa matibabu ya afya kupitia utaratibu wa  Mfuko wa afya wa Jamii(CHF) iliyoboreshwa utakaoendana na utoaji wa kadi za bima kuanzia ngazi za vitongoji, unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa Juni mwaka huu nchini kote.

Hatua hiyo inatokana na kuendelea kukamilika kwa mchakato wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa kada mbalimbali katika sekta ya afya ambao watahusika kwa namna moja au nyingine kusimamia mpango huo ambapo inaelezwa mpango huo utatoa fursa kwa wakazi wa majiji na halmashauri kunuifaka na CHF iliyoboreshwa ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha wanananchi wanakuwa kwenye mfumo wa kulipia matibabu kabla ya kuugua kwa kutumia kadi ya kadi za afya.

Hayo yalibainishwa na Katibu wa Afya mkoa wa Dar es Salaam Sister Mathew wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa watumishi mbalimbali wa idara ya afya wakiwemo waganga  wakuu wa hospitali za wilaya pamoja na wataalamu katika mifumo ya utoaji wa  huduma hizo.Lengo la mafunzo hayo ilikuwa ni kuwajengea uwezo watumishi hao ili kuhakikisha unafanikiwa.

Mathew amefafanua kwa kuzingatia umuhimu wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi nchini  kote, Serikali ilifanya majaribio ya mpango huo katika hospitali zote zilizopo mikoa ya Dodoma, Shinyanga na Morogoro na kutoa mafanikio, hatua iliyoilazimu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto kuja na mkakati huo kwa nchi nzima kupitia CHF iliyoboreshwa.

Amesisitiza wanaamini kuanza kwa utaratibu huo utawawezesha wananchi kupata kadi za afya kuanzia ngazi za zahanati zilizopo katika  vitongoji vyao na kwa asilimia kubwa utasaidia kuondoa changamoto kwa wananchi na watakuwa na uhakika wa kupata matibabu ya afya ya uhakika tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Mathew pamoja na mpango huo, kuanzia sasa huduma za utoaji wa kadi za matibabu kupitia utaratibu wa bima za CHF, utamwezesha mwananchi kupata matibabu kupitia vituo vyote vya afya tofauti na hapo awali ambapo utaratibu ulimtaka mwananchi kupata huduma kupitia kituo alichojiandikisha.

"Baada ya kuanzishwa kwa utaratibu wa usimamizi wa mapato unaolenga uboreshaji wa huduma za afya katika hospitali zote kuanzia ngazi za vitongoji, tunaamini utasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya ukichangiwa na mpango wa ushirikishwaji wa sekta binafsi ‘Public Private Patnership’ (PPP),"amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa ‘Public Private Patnership’(PPP) kutoka Wizara ya afya Maendeleo ya Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Dk.Mariam Ongara,  pamoja na mambo mengine amesema uboreshaji huo unaoenda kufanyika katika vituo vyote vya afya na utasaidia kupunguza urasimu na kuimarisha uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya kupitia CHF iliyoboreshwa.

Aidha amesema utaratibu huo wa ugatuaji  unahusisha utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za afya (direct health facility financing) hatua itakayoviwezesha vituo vyote vya afya kujiendesha hususani kwa kuwa na dawa na vitendanishi vya kutosha na hivyo kusaidia utoaji wa huduma za uhakika kwa wananchi.

Alisema  hatua hiyo pamoja na mambo mengine, inachangiwa na utaratibu wa Wizara hiyo, uliowezesha  kuajiriwa kwa wahasibu 300 waliosambazwa katika vituo mbalimbali nchini ili kuimarisha usimamizi wa fedha zinazopatikana ambazo zitatumika kusaidia uboreshaji wa huduma katika vituo vyote vya afya katika mikoa 23 nchini.

Akifafanua kuhusu matibabu ya afya kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa familia ya watu sita itaweza kujiunga kwenye utaratibu huo kwa kulipia Sh.150,000 kwa mwaka na kwa mtu mmoja itakuwa Sh.40,000. Alipoulizwa je Dar es Salaam na majiji mengine nayo yatakuwa kwenye mpango huo amefafanua mpango huo utahusisha na jiji hilo na maeneo mengine yote nchini.

Sababu ya kuulizwa swali hilo ilitokana na maelezo ya baadhi ya waandishi kuwa CHF imekuwepo kwenye baadhi ya halmashauri mikoani na kwa Dar es Salaam utaratibu huo haukuwepo.

"Niwahakikishie wananchi wote wakiwamo wa Dar es Salaam mpango wa CHF iliyoboreshwa utaanza rasmi kati ya Juni mwanzoni au Julai na hivyo kinachoendelea sasa ni maandalizi ya kufanikisha azma hiyo na ndio maana tumenza na mafunzo kama moja ya hatua ya kuelekea ambapo tumedhamiria kwenda kwa kutoa huduma bora za afya kwa mfumo wa kadi ya bima ya afya,"amesema Dk.Ongara.
Mkufunzi Ally kebby akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafunzo ya mpango wa utoaji huduma wa CHF iliyoboreshwa ambayo wameyatoa kwa watumishi mbalimbali wa sekta ya afya mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wakipatiwa mafunzo kuhusu namna ya kutoa huduma za Afya kupitia Mpango wa Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF)iliyoboreshwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad