HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 11, 2018

BODI YA MIKOPO YAFAFANUA KUHUSU UMILIKI WA LESENI ZA BIASHARA KWA WAZAZI SIO SIFA YA MWANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KUKOSA MKOPO

Tunapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zisizo za kweli zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa waombaji wa mikopo ambao wazazi wao wanamiliki leseni za biashara hawatapata mikopo ya elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2018/2019. Taarifa hizo sio sahihi na zinapotosha waombaji mikopo na umma kwa ujumla.

Ufafanuzi wa kina ni kama ifuatavyo:

a)   Mikopo inayotolewa na Serikali kupitia HESLB inaongozwa na Sheria ya HESLB (SURA 178) pamoja na Mwongozo unaotaja sifa, vigezo na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo. Mwongozo huu unapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na hautaji kigezo cha umiliki wa leseni kama sifa ya kukosa mkopo;

b)   Pamoja na mwongozo huu, HESLB pia imeandaa kitabu kwa lugha nyepesi ya kiswahili chenye Maswali na Majibu 21 ili kuwawezesha waombaji mikopo kufahamu sifa na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo kwa ukamilifu na usahihi. Kitabu hiki pia hakijataja umiliki wa leseni kwa mzazi au mlezi kama sifa ya mwanafunzi kukosa mkopo;

c)    HESLB inaamini umiliki wa leseni ya biashara kwa wazazi ni jambo jema na linapaswa kupongezwa kwa kuwa linaimarisha mifumo ya utambuzi kwa wafanyabiashara.

Bodi ya Mikopo inapenda kuwakumbusha wadau wote, wakiwemo wazazi, walezi na wanafunzi waombaji wa mikopo kusoma kitabu cha mwongozo wa utoaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 na kitabu chenye maswali 21 ambavyo vinapatikana katika tovuti (www.heslb.go.tz).

Vitabu hivi ndiyo nyaraka rasmi za HESLB zinazotoa mwongozo kuhusu maombi ya mikopo kwa mwaka 2018/2019. Aidha, HESLB inapenda kuwakumbusha wadau wote, wakiwemo wanahabari, kusoma nyaraka hizo na kutumia kalamu na kamera kuwaelimisha waombaji mikopo kwa usahihi.



Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad