Na Bathromeo C. Chilwa
Afisa Habari Halmashauri ya wilaya Geita
Mkuu wa Mkoa Geita Mhandisi Robert Gabriel ametoa siku saba kwa wazazi wa wanafunzi 1,957 wa shule za sekondari thelathini katika Halmashauri ya wilaya ya Geita walioacha shule na kwenda kufanya kazi za majumbani, mahotelini,uvuvi na migodini kuhakikisha watoto hao wanarudi shule la sivyo mkono wa sheria utawafikia.
Ameyasema hayo katika kata ya Ludete wakati akipokea msaada kutoka benki ya NMB wa Mashuka 54, Vitanda 7, na Magodoro 7 kwa ajili ya kituo cha afya Katoro pia Mabati 204 yatakayopaua vyumba vinne vya madarasa vya shule mpya ya Sekondari Kilimahewa yenye maboma 18 yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi wa kata ya Ludete.
“DC na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ninawaomba msimamie hili na mhakikishe mnawakamata wazazi na wananchi wote wanaotumikisha wanafunzi katika shughuli mbalimbali hasa majumbani. Pia wanafunzi waliozeshwa kwa makubaliano ya wazazi wao na wale waliwatorosha watoto wakamateni wazazi hao na wawekeni ndani mpaka watoto watakapopatikana na kurudi shuleni” RC Gabriel amesisitiza
Kwa upande wa diwani kata ya Ludete Mheshimiwa Sebastian Mlando amesema changamoto nyingi ndani ya kata zinatatuliwa kwa ushirikiano wa Halmashauri,Wadau wa maendeleo, wenyeviti wa vitongoji na wananchi kwa ujumla na kwa kipindi kifupi cha miaka miwili kata ina maboma 34 ya shule za sekondari. Ludete yapo 16 na shule ya sekondari Kilimahewa yapo 18, Pia ujenzi wa vyumba vya madarasa (maboma) 16 kwa shule za msingi tatu ukiendelea, ukarabati wa zahanati na ujenzi wa Kituo kipya cha afya .
Halmashauri ya wilaya ya Geita ina jumla ya shule za sekondari 30 ambapo kwa mwaka 2017 takwimu zinaonyesha wanafunzi waliosajiliwa walikua 18,540 wasichana wakiwa 8,045 na wavulana wakiwa 10,495 ambao wanaohudhuria shuleni wasichana ni 7,126, wavulana 9,133 jumla yao ni wanafunzi 16,259 sawa na asilimia 88% kwa upande wa wasiohudhuria shuleni ni wasichana 774 na wavulana 1,183 wakiwa na jumla ya wanafunzi 1,957 sawa na asilimia 11 % ya wanafunzi wote waliosajiliwa.
No comments:
Post a Comment