Uongozi wa klabu ya Simba umesema unaamini kabisa waamuzi wa mechi yao dhidi ya Yanga Jumapili, watatenda haki.
Klabu hiyo kupitia kwa Afisa habari wao, Haji Manara amesema hawatawalalamikia waamuzi kabla lakini wanaamini kikubwa ni haki na zaidi waamuzi wengi ni vijana na wanajua maana ya mchezo wa haki.
“Waamuzi watakaocheza tunaamini watafuata sheria 17 za soka kwa ajili ya kufanya haki itendeke,” alisema.
Manara amesema kuwa mpaka sasa kikosi chao hakina majeruhi hata mmoja kikosini kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao, Yanga utakaopigwa kwenye dimba la Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Simba wakiwa vinara wa ligi hiyo kwa pointi 59 kutokana na mechi 25, watakuwa wenyeji wa mchezo huo dhidi ya Yanga waliopo nafasi ya pili na pointi 48, huku wakiwa wameshuka dimbani mara 23.
Simba inashuka dimbani Jumapili kuivaa Yanga katika mechi ambayo kama watashinda, basi watakuwa wamejihakikishia kubeba ubingwa kwa asilimia 95.
Manara amesema kwamba maandalizi yanaendelea vizuri baada ya kikosi cha timu hiyo kurejea wakitokea Morogoro walipoweka kambi ya siku tatu.
Amesema taarifa kutoka benchi la ufundi kwamba kikosi hicho kinaendelea vizuri na tayari kwa ajili ya mchezo huo kwa kuhakikisha wanapata pointi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya mbio za ubingwa.
“Hadi leo hakuna majeruhi na timu inaendelea na mazoezi yake katika Uwanja wa Boko na kikubwa tunawaomba waamuzi kuzitendea haki kanuni na sheria za soka, waepuke kuingia na matokeo yao mfukoni,"alisema Manara.
Manara amesema anaiheshimu Yanga haswa kuelekea katika pambano hilo la watani wa jadi, hivyo huenda wasipate ushindi ila wanaenda kutafuta pointi muhimu katika mchezo huo.
“Tuna imani ya timu yetu inaweza kuchukuwa ubingwa, lakini sio kama tutashinda mechi zote, mashabiki watambue kwamba kuna mechi tutapoteza, lakini kikubwa wachezaji wanapambana kuhakikisha tunafikia malengo yaliyokuwepo tangu awali,” amesema Manara.
No comments:
Post a Comment